October 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Sina hofu yoyote ushindi ninao – OMO

 

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman ametoa nasaha zake muhimu kwa Wanachama na viongozi waandamizi wa chama chake kwa kuzindua timu za ushindi (TIMU OMO) upande wa kisiwani Pemba leo tarehe 20 Oktoba 2025, kwenye ukumbi wa chama Mkoa wa Kichama Chake Chake, Pemba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba … (endelea).

“Mimi nimeshaandaa serikali yangu. Ni kwa sababu najua ninao watu thabiti wa kuzilinda kura na kwa ujumla ushindi wetu katika uchaguzi mkuu huu,” aliwaambia viongozi hao wakiwemo wakuu wa Ngome zote tatu ndani ya chama hicho.

“Nina imani kubwa nanyi. Mjitambue kwamba nyie ni jeshi langu kubwa na mimi niwaahidi sitawaangusha katika matarajio yenu,” anasema.

Othman aliyewasili kisiwani Pemba asubuhi ya leo akitarajiwa kumaliza awamu ya kampeni za uchaguzi mkuu, alishuhudia wanachama wakiwa na morali ya hali ya juu kusubiri siku ya uchaguzi kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Viongozi walioongoza timu hizo ni Fatma Abdulhabib Fereji [Wanawake]; Mohamed Busara [Vijana] na Janeth Medard Fussi [Wazee]. Wengine ni wenyeviti na makatibu wa majimbo 18 yalioko Pemba pamoja na Kamati za Uongozi [KU] za mikoa minne ya kichama Pemba – Micheweni, Wete, Chake Chake na Mkoani.

Ziara ya Othman ambaye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, itajumuisha pia mikutano ya Hadhara, vikao na Mawakala pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi kisiwani humu, ikiwa ni muendelezo wa ada yake.

Baadaye leo Othman anatarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara wa kampeni jimbo la Ole.

About The Author

error: Content is protected !!