
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa mvua za msimu (Novemba, 2025 hadi Aprili, 2026) mahususi katika mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka, ambapo msimu huu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha katika maeneo mengi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk. Ladislaus Chang’a amesema maeneo hayo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unatarajiwa kuanza mwezi Novemba na kuisha kati ya mwezi Aprili na Mei ya mwaka unaofuata.
Dk. Chang’a amesema mikoa ambayo inapata mvua za msimu ni katika maeneo ya magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi), kanda ya kati (mikoa ya Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini magharibi (mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa), kusini mwa nchi (mkoa wa Ruvuma), ukanda wa pwani ya kusini (mikoa ya Lindi na Mtwara) pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Amesema kutokana na mifumo ya hali ya hewa mvua hizo za msimu zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida na Dodoma, lakini mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara na Lindi pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Dk. Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba, 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma; na kusambaa katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2025.
Katika Pwani ya kusini na maeneo ya kusini mwa nchi: (Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma), mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Desemba, 2025 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili na ya kwanza ya mwezi Mei, 2026.
Amesema mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2026 katika maeneo mengi yanayopata mvua za msimu.
Dk. Chang’a amesema ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha nusu ya pili ya msimu unaonza mwezi Februari mpaka Aprili, 2026 ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwezi Novemba, 2025 mpaka Januari, 2026.
Pamoja na mvua hizo kuwa za wastani hadi chini ya wastani, Dk. Chang’a ametoa angalizo uwepo wa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.
Dk. Chang’a amewashauri wadau kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waweze kujua mabadiliko yanayotokea katika mifumo ya hali ya hewa kwa kila siku.
ZINAZOFANANA
Mahakama Kuu yakataa Kibatala, mdogo wa Polepole kuhojiwa
JWTZ latoa tamko kuelekea Uchaguzi Mkuu
Isingewezekana Mpina kupata haki – Shahidi wa serikali kesi ya Lissu