October 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

OMO aahidi kupitia upya mfumo wa mafao ya wastaafu serikalini

 

MGOMBEA Urais wa Chama cha ACT Wazalendo ameahidi kuwa Serikali yake, endapo itapata ridhaa ya wananchi, itapitia upya mfumo mzima wa mafao ya wastaafu Serikalini ili kuhakikisha wastaafu wanapewa heshima, thamani, na haki zao za msingi kwa mujibu wa mchango wao katika kulitumikia Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza na wazee wa Jimbo la Kiwani, Wilaya ya Mkoani, kisiwani Pemba, mgombea huyo alisema kuwa hali ya wastaafu kwa sasa ni ya kusikitisha, kwani wengi wao wametelekezwa, kudharauliwa, na kuteseka licha ya kufanya kazi kwa uaminifu na bidii kubwa kwa miaka mingi.

Amesema wastaafu wamefanya kazi kubwa kwa moyo wa uzalendo, lakini leo hawathaminiwi. Serikali yake itahakikisha kila mstaafu anapewa thamani anayostahili, na jasho lao linawafaidisha wao na familia zao.

Ameongeza kuwa mfumo wa sasa wa hifadhi ya jamii, hususan kupitia Mfuko wa ZSSF, umekuwa kero kubwa kwa wastaafu badala ya kuwa suluhisho la maisha yao baada ya kustaafu.

Amesema mfuko wa ZSSF kwa sasa umekosa maana kwa wastaafu. Badala ya kuwasaidia, umekuwa kama chombo cha kuwanyonya.

Kikotoo kinachotumika kuwalipa wastaafu hakiendani kabisa na hali halisi ya maisha.

Mgombea huyo amesema serikali ya ACT Wazalendo itapitia upya kanuni, mifumo ya kikotoo, na utaratibu wa mafao kwa lengo la kurejesha imani kwa watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu. Alisema ni lazima haki, utu, na heshima ya mstaafu vilindwe kwa nguvu zote.

Aidha, ameahidi kuwa katika Serikali yake, wastaafu watashirikishwa moja kwa moja katika maamuzi yanayohusu maslahi yao, na kuwepo kwa mfumo wa malipo wa haraka na wa haki unaozingatia thamani halisi ya mchango wa kila mtu.

Amesema Serikali yake haitakubali kuona mzee anahangaika kupata haki yake ya msingi. Wastaafu ni nguzo muhimu ya taifa na ni lazima waheshimiwe na kuenziwa.

Kwa upande wao, wazee wa Kiwani wamepongeza kauli hiyo ya mgombea huyo na wamesema wamefahamu kwa kina dhamira njema aliyonayo katika kuleta mageuzi Serikalini.

Wamesema ahadi zake zinaonesha uhalisia na upendo kwa wananchi wote, hususan wazee na wastaafu.

Wamesema kwa muda mrefu wastaafu wa Serikali wamekuwa wakipitia mateso makubwa, huku haki zao zikicheleweshwa au kupotea kabisa.

Wamepongeza ahadi ya ACT Wazalendo ya kubadilisha mfumo huo na kuahidi kumpa mgombea huyo ushirikiano wa karibu katika kampeni zake.

Wazee hao pia wameahidi kumpa kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao, wakisema wanataka kuona Serikali yenye utu, usawa na inayowajali wastaafu wote wa Zanzibar.

About The Author

error: Content is protected !!