October 8, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu aibua mapya mahakamani

 

GEORGE Bagyemu, Naibu Mkuu wa Upelelezi (ASP), Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, amedai kuwa Freeman Mbowe, aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa miongo miwili, ni mtu muhimu mno kwa serikali, kuliko mrithi wake, Tundu Antipas Lissu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Afisa huyo wa polisi amedai pia kuwa hafahamu kama Lissu, aliwahi kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, mjini Dodoma, wakati akitokea bungeni na kupatiwa matibabu jijini Nairobi, nchini Kenya na Ubelgiji.

Aidha, George amekiri kuwa hakuwahi kumjulisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TIS), wala Mkuu wa Usalama wa taifa mkoa wa Dar es Salaam (RSO) na hakumjulisha Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP), kabla ya kufungua kesi ya uhaini.

Vilevile, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi, amekiri kufanya kazi Rufiji, wakati ambapo jeshi la polisi lilituhumiwa kuendesha mauaji ya watu mbalimbali, katika kile walichokiita, “…mapambano dhidi ya ugaidi.”

George alitoa kauli hiyo leo, tarehe 8 Oktoba 2025, mbele ya majaji wa Mahakama Kuu, alipokuwa akijibu maswali ya dodoso, yaliyoulizwa na Lissu, wakati wa kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi huyo wa upinzani.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Mstaafu wa Chadema

“Yule Mbowe,” George anasema, “Ni mtu muhimu kuliko wewe.”

Katika hatua nyingine, shahidi huyo wa kwanza wa Jamhuri kwenye kesi hiyo ya uhaini, Na. 19605/2025 dhidi ya Lissu, ameiambia mahakama kuwa hakutumia kamusi ya Kiswahili sanifu kutafsiri neno uasi.

Mapema Lissu alimuuliza George, nini maana ya uasi na kumtaka kusoma Kamusi ya Kiswahili, Toleo la 3 inayotaja kuwa ni tendo la kuvunja sheria, kanuni au amri.

“Kamusi ya Kiswahili sanifu imetolewa na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na hii inasema tolea la 2002 inasema uasi hali ya uvunjaji wa kanuni, sheria au amri,” alieleza Lissu.

Akahoji: “Sasa swali je wewe unafahamu maana tofauti ya hizi zilizopo kwenye kamusi?” George akasema, “Hizo tafsri zipo vizuri nakubali.”

Alipoulizwa kama kuna sheria inayozuia mikutano ya hadhara na kwamba iwapo mtu akivunja sheria hiyo, atakuwa amefanya uasi, George haraka alijibu: “Haliwi kosa la uhaini.”

Kuhusu kufanya maandamano bila kutoa taarifa polisi, George alijibu: “Nalo sio kosa la uhaini.”

Alipoulizwa iwapo mtu atavunja sheria ya uchaguzi, anaweza kushitakiwa kwa makosa ya uhaini, George alisema, “Kwa hilo haiwezekani, lakini wewe ulitishia serikali.”

Tundu Lissu: Ninayo hapa Sheria ya Uchaguzi wa Rais wabunge na madiwani ya mwaka 2024, Sura ya 7 inazungumzia makosa na adhabu zake. Sasa wambie majaji kosa la kwanza ni kosa gani?

George: Makosa yanayohusu uandikishaji wa wapiga kura.

Tundu Lissu: Hili ni kosa la uhaini?

George: Hapana.

Tundu Lissu: Nitakuuliza yote ili nikienda kunyongwa niseme hakuna swali niliacha kuuliza.

Tundu Lissu: Kosa la pili ni nini?

George: Kutumia wadhifa kushawishi wasiombe kuteuliwa.

Tundu Lissu: Katika yote uliyosoma kwenye sheria hiyo, kuna kosa la kuzuia uchaguzi mkuu?

George: Lipo kwenye makosa mengineyo.

Tundu Lissu: Hebu yaseme.

George: Makosa mengineyo maana yake ni kusema uongo na adhabu yake ni kulipa faini shilingi elfu hamsini (50,000).

Akizungumzia ukubwa wa mashitaka yanayomkabili na adhabu itakayotolewa pale atakapopatikana na hatia, Lissu alisema, hatakubali kunyongwa kizembe.

Kwa mujibu sheria, iwapo Lissu atapatikana na hatia, atakabiliwa na adhabu ya kunyongwa hadi kufa. Akimbana shahidi huyo, Lissu alisema: Kwa hiyo, katika orodha ya makosa yote ya uchaguzi hakuna kosa la kuzuia uchaguzi?

George: Kwa niliyoyasoma hakuna hilo kosa, lakini sehemu nyingine linaweza kuwepo.

Tundu Lissu: Hayo mengine baki nayo mwenyewe, mimi nimekupa sheria. Mtu hawezi kwenda kunyongwa bila mapambano, hilo nakuahidi.

Tundu Lissu: Atakinukisha vibaya sana tena sana. Nilisema hivyo?

George: Ndio.

Tundu Lissu: Kwenye maelezo yako uliyanukuu hayo maneno, kwamba wanasema msimamo huu unaashiria uasi, tutakwenda kukinukisha sana sana.

Je, katika maelezo yako yote ulifafanua maana ya maneno tutakinukisha vibaya sana au tutakinukisha sana?

George: Sikutafsiri neno moja moja.

Tundu Lissu: Unafikiri ni rahisi kunyonga mtu. Haya maneno kwenye hati ya mashitaka kuna mahali hayo maneno tutakinukisha yametafsiriwa?

George: Kwa neno moja moja hayajatafsiriwa.

Tundu Lissu: Sasa twende kwenye Kiswahili sanifu tukaone maana ya neno kukinukisha. Tuangalie sasa maana ya neno ‘kukinukisha,’ ni sahihi neno kukinukisha linatokana na neno nuka au nukia?

George: Ni sahihi.

Lissu: Kamusi inasema tokwa na harufu mbaya au vunda na nukia ni toa harufu nzuri. Kamusi nyingine ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam inasema nuka ni toa harufu mbaya kwasababu ya kuoza.

Nukia toa harufu nzuri kama vile marashi. Sasa kama tulisema tutakinukisha sanasana maana yake kinuke vibaya kitoe harufu mbaya sana si kweli?

George: Kwa unayosoma kwenye kamusi ni kweli kabisa.

Tundu Lissu: Navilevile kukinukisha kinukie, ni kukifanya kitoe harufu nzuri sana?

George: Kwa vile ulisema vibaya basi ni kinuke sio kunukia.

Tundu Lissu: Na kukinukisha sana sana, inaweza kuwa kinukie vizuri sana?

George: Hiyo haiwezekani.

Kuhusu ASP George kushiriki operesheni za Rufiji, shahidi huyo alikiri ushiriki wake na akakiri kwamba watu wengi waliuawa kwenye operesheni hizo.

Miongoni mwa wanaoaminika kuwa huenda wameuawa kwenye operesheni ya Rufiji, ni pamoja na Azory Gwabda, mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Citizen.

About The Author

error: Content is protected !!