
Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chadema akiwa mahakamani
MAHAKAMA kuu Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imeanza kusikiliza ushahidi kwenye shauri la Uhaini linalomkabili Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu. Anaripoti mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Zoezi hilo la kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo namba 19605/2025 limefunguliwa na ofisa wa jeshi la Polisi Kamishna msaidizi ASP George Wilbard Bagyemu (48), ambaye anafanya kazi chini ya Faustine Mafwele, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam (ZCO), amekuwa shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga , mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa , Jaji Dunstan Ndunguru, na akishirikiana na Jaji James Karayemaha, na Jaji Ferdinand Kiwonde alidai mahakamani hapo kuwa Lissu alitoa maneno yanye kuashiria jinai.
ASP Bagyemu amedai mahakamani hapo kuwa yupo kwenye jeshi hilo kwa muda wa miaka 22 sasa kwamba alianza kazi tangu Aprili mwaka 2003
Amekitaja kwa urefu cheo cha cha ASP kwamba ni Kamishna Msaidizi wa Polisi alichokuwa nacho tangu Juni 2025 ambapo kabla alikuwa Mrakibu Mwandamizi wa jeshi hilo SSP na kwamba alikuwa Kontebo wa Polisi tangu tarehe 28 Aprili 2003.
“Baada ya hapo mwaka 2006 January niliteuliwa kwenda kwenye mafunzo ya Assistance Inspector Of Police Course. (Mkaguzi Msaidizi wa Polisi) nilivyofaulu na kuhitimu nikapandishwa cheo na kuwa ASP yaani Assitant Inspector of Police,” alidai.
Bagyemu, ameieleza mahakama kuwa majukumu yake ya sasa ni kumsaidia Mkuu wa Upelelezi kanda ya Dar es Salaam, Kuwaongoza maafisa na wakaguzi na wapelelezi, kusimamaia mashauri yote yaliyofunguliwa , na kupeleleza mashauri ya jinai na shughuli nyingine za kiupelelezi ndani ya Kanda.
Amedai kuwa tarehe 4 Mei 2025 akiwa ofisini kwake pia akikaimu ukuu wa upelelezi wa kanda kwa sababu wakati huo ZCO alikuwa nje ya Dar es Salaam.
Amedai kuwa siku hiyo majira ya saa nne asubuhi Askari ASP John Kahaya anayefanya kazi kwenye dawati la doria mtandaoni aliingia ofisini kwake na kumueleza kuwa akiwa kwenye shughuli zake aliona picha mjongeo (video) kwenye Youtube ya Jambo TV yenye kichwa cha habari ‘Tundu Lissu, uso kwa uso na watia nia No Reforms No Election.
“Akanieleza katika picha hiyo mjongeo maudhui yake yalikuwa na ujinai ndani yake. Nilimtaka anioneshe na mimi, akiwa na simu yake janja aliingia YouTube ya JAMBO TV akaanza kunionesha sehemu ya hiyo picha mjongeo na sehemu zinazohusu maudhui ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu,” amedai.
Amedai kuwa Kahaya alimuonesha video hiyo na anakumbuka kuna maneno aliyesema Lissu kwamba Polisi kubeba vibegi mgongoni vyenye kura feki na kwenda navyo kwenye vituo vya kupigia kura.
Lissu akiingilia na kudai kuwa ushahidi wa vibegi hauhusiani na mashtaka yake, “haya ya vibegi ushahidi wake ufutwe maana hakuna kokote kunakohusiana na mimi kusema vibegi kwenye mashitaka wasome section 7 and 8 ya sheria ya ushahidi,” ameeleza Lissu.
Wakati huo huo, naye Katuga akaeleza kuwa wachwe Jamhuri wathibitishe kesi hiyo bila kuacha yoyote.
Baada ya mabishano hayo mahakama hiyo imemruhusu ASP Bagyemu kuendelea na ushahidi wake.
Amedai kuwa akamtafuta shahidi mwingine ambaye mahakama imetoa amri mashahidi hao wafichwe aliyepewa jina la ‘P’ na kwamba aliwasiliana na Kamishna Msaidizi wa Polisi aliyekuwepo makao makuu ya Polisi Dodoma alimtaja kwa jina la DCP Ng’anzi kumjulisha kuwa shahidi aliyekuwa kwenye tukio na kifaa kilichotumika kurekodi vyote vipo Dodoma.
“Nikamtajia DCP Ng’anzi namba za simu za P ili tupate maelezo yake na zile picha mjongeo kwa maana ya kupata kifaa kilichotumika kupata picha hiyo mjongeo,”amedai.
Amedai kuwa tarehe 7 Aprili walikabidhi video aliyoipakua kutoka kwenye mtandao wa kijamii YouTube ya Jambo TV yenye ushahidi kwenye flash diski
“Nikaanza kumpa Reference ya kesi ya PI ile nimeitaja mwanzo. Ili flash disk hiyo pamoja na PF 145 yaani Exhibit label ili hicho kielelezo kiweze kutunzwa kwa mtunza vielelezo ambae ni ASP Peter Malugala,”amedai.
“Tarehe hiyo hiyo (7 Aprili) nakumbuka Afande DCP Ng’anzi alinieleza kuwa maelezo ya P ambaye alirekodi maelezo yake pamaoja na memory card ikiwa kwenye card reader vimepatikana ilikuwa ni majira ya saa 10 au 11. Akasema ASP Churu atakuja navyo vitu hivyo huku Dar es Salaam na kuleta maelezo yake,” ameendelea kudai.
Amedai kuwa alielekeza kufunguliwe kwa majalada mawili ikiwemo na uhaini na kuchapisha taarifa za uongo “Baada ya hapo nikajua sasa picha mjongeo ni picha halisi na haikuwa imetengenezwa baada ya kulijua hilo. Tarehe 8 Aprili 2025 nilielekeza majira ya asubuhi, ASP Michael afungue majalada mawili la uhaini na kuchapisha taarifa ya uongo mtandaoni.
“Matokeo yake lilifunguliwa jalada la uhaini CDS/IR/727/2025 na jalada la pili lilikuwa ni CDS/IR/761/2025.
Nilisema kosa ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Nilibaini picha ile mjongeo ni halisi. Nilishapata wasaa wa kuyaangalia kutoka YouTube wa Jambo TV. Ilikuwa na urefu wa masaa matatu hivi”
Shahidi huyo alieleza kuwa baadhi ya maneno yaliyomfana aone kuwa kuna viashiria vya jinai ni maneno yaliyosemwa na Lissu kwamba atahamasisha uasi na atazuia uchaguzi.
“Nilivyoangalia niliona ni kosa la uhaini kwa sababu Tundu Lissu alisema atahamasisha uasi, atazuia uchaguzi, atakinukisha sana sana, atavuruga kweli kweli na atakinukisha vibaya sana,” amedai ASP Bagyemu.
Amedai kuwa maneno hayo Lissu aliyatoa kwa nia ya kuitishia serikali.
ASP Bagyemu alihitimisha kuwasilisha ushahidi wake na kwamba kesho tarehe 7 Oktoba itakuwa zamu ya upande wa utetezi ambapo Lissu ameamua kujitetea mwenyewe atamuuliza maswali shahidi huyo.
ZINAZOFANANA
Hukumu kesi ya Mpina, INEC kutolewa Alhamisi
Lissu asimamisha mahakama kisa tarehe ya hukumu yake kabla ya kusikilizwa
Mahakama yafafanua mashtaka ya Lissu kuhusu hukumu yake