
MGOMBEA urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman ‘OMO’, leo tarehe 30 Septemba 2025, ameanza safari kutoka Unguja kuelekea kisiwani Pemba kwa ajili ya ziara ya siku saba yenye lengo la kujenga ushawishi na kupata ridhaa ya wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pemba … (endelea).
Katika ratiba ya ziara hiyo, Othman anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ya Pemba, akizungumza na wananchi juu ya changamoto zinazowakabili na kutoa dira ya ACT, kwa Zanzibar mpya.
Vilevile, ataendesha mazungumzo na viongozi wa dini, viongozi wa kijamii pamoja na watu mashuhuri, akiwashirikisha moja kwa moja katika mchakato wa mabadiliko.
Akizingatia mchango wa kilimo, hasa kilimo cha viungo, Othman atakutana na wakulima ili kujadiliana nao njia za kuongeza thamani ya mazao na kuyageuza kuwa chanzo kikuu cha uchumi wa Zanzibar.
Pia, atakutana na wazee wa Pemba akiwapa heshima na nafasi ya kutoa busara zao kwa mustakabali wa taifa.
Akizungumza kabla ya kuondoka Unguja, Othman alisema:
“Ziara hii ni ya kuwasikiliza wananchi wa Pemba na kupata maoni yao moja kwa moja. Tunataka kujenga Zanzibar ya usawa, mshikamano na maendeleo ya kweli, ambapo kila Mzanzibari ataona matunda ya rasilimali zake. Huu ni wakati wa kuikomboa nchi yetu na kuirudisha mikononi mwa wananchi,amesema Othman”.
Ziara hii imeelezwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa ni hatua ya kimkakati inayoongeza mvuto wa Othman kwa wananchi wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla, huku akionekana kama kiongozi anayeibua matumaini mapya kwa wananchi waliochoshwa na changamoto za muda mrefu.
ZINAZOFANANA
Busara za Maalim Seif nguzo ya kuinusuru Zanzibar – Othman Masoud.
Polepole kumwaga mboga Jumanne
Uchaguzi mkuu ujao: Kupata au kupatwa?