
HILO ndilo swali ambalo wananchi wanajiuliza, wakati huu ambako Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hii ni kwa sababu, taifa hilo linakabiliana na kipimo kingine cha kuthibitishia ulimwengu kuwa demokrasia yake bado iko imara na inaendelea kupanuka.
Kwa mfano, uchaguzi mkuu unafanyika wakati kiongozi wa chama kikuu cha upinzani (CHADEMA), Tundu Lissu, amezuiliwa gerezani kwa tuhuma za uhaini.
Hii ni baada ya chama chake, kutangaza kupitia mkutano mkuu wa 21 Januari mwaka huu, kwamba hakitashiriki uchaguzi mkuu ujao, bila kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi.
Mkutano mkuu wa Chadema, ulikwenda mbali zaidi kwa kusema, mifumo ya uchaguzi iliyopo nchini Tanzania, inakipendelea chama tawala yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Swali ambalo wananchi wanajiuliza ni hili: Kutoshiriki kwa Chadema kwenye uchaguzi huo, kunaweza kuleta athari gani?
Kwanza, Chadema siyo chama cha kwanza hapa Tanzania, kuchukua mkondo huu wa kisiasa, ili kukabiliana na chama kilichoko madarakani.
Machi 2016, Chama cha Wananchi (CUF), kilisusia uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika baada ya Tume ya Uchaguzi, chini ya Jecha Salum Jecha, kuamua kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2015.
Hoja ya CUF wakati ule ilikuwa kwamba kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa, chama chao kilikuwa kimepata ushindi na badala ya kurudia uchaguzi, kilichotakiwa kufanyika ni kuhesabu upya kura kutoka vituoni.
Kilichofuata baada ya uchaguzi wa marudio ni CCM kutangazwa mshindi kwa asilimia 91 ya kura zilizopigwa.

Kwa Zanzibar, aina hii ya ushindi kwa chama kimoja ilikuwa haijawahi kutokea tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
Kilichofuata ni kwamba mafanikio yaliyopatikana kupitia mwafaka wa mwaka 2010 na kufanikisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), vyote vilipeperushwa na uchaguzi wa Machi 2016.
Aidha, kilichotokea Zanzibar mwaka 2016 kinafanana na kilichotokea nchini Ethiopia wakati wa utawala wa Mengistu Haile Mariam miaka ya 1980 na enzi za Meles Zenawi kwenye miaka ya 1990.
Vyama vikuu vya upinzani vilisusia uchaguzi na kutoa fursa kwa chama tawala kujisimika zaidi madarakani pasipo kufanya mabadiliko yaliyokuwa yanatakiwa.
Kimsingi, tafiti mbalimbali za wataalamu wa sayansi ya siasa zimebainisha kwamba barani Afrika, kitendo cha wapinzani kususia uchaguzi – iwe Ivory Coast au Mauritania, Uganda, Kenya, Nigeria au Sudan, faida kwa upinzani huwa ni ndogo kuliko kwa chama kilicho madarakani.

Watanzania wamelalamikia Bunge la 2020 – 2025 kwamba lilikuwa dhaifu. Kuna uwezekano mkubwa wa Bunge lijalo kufuata mkondo huo huo.
Pili, ili kususia uchaguzi kufanikiwe, kuna mambo kadhaa yanatakiwa yawepo kwa mujibu wa wasomi wa masuala ya sayansi ya siasa.
Kuwe na vyama vya upinzani vyenye nguvu, kuwe na asasi imara za kiraia na kuwe na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa.
Tatizo la nchi kama Tanzania ni kwamba kwa sasa – hasa baada ya miaka sita ya utawala wa John Magufuli, hali ya vyama vya siasa ni dhoofu.
Vina upungufu mkubwa wa rasilimali fedha, rasilimali watu na mibinyo ya kimfumo, pamoja na baadhi ya viongozi wake, kujigeuza madalali wa chama tawala.
Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa imani ya wananchi kwa Chadema imeongezeka mara dufu.
Hii inatokana na uamuzi wa chama hicho wa kung’ang’ania msimamo wake wa No Refoms, No Election – yaani “Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi.”
Kingine kilichokipaisha chama hicho, ni kukamatwa kwa Lissu na kuanguka kwa Freeman Mbowe, kwenye uchaguzi huru na wazi wa Januari mwaka huu.
“Hata uamuzi wa waliokuwa wafuasi wa Mbowe, wakiwamo mtoto wake, James Mbowe, kuondoka Chadema na kujiunga na Chaumma, baada ya Lissu kushinda uchaguzi, kumekiongezea chama hicho, kukubalika kwake kwa umma,” anaeleza Mohammed Seif, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam.
ZINAZOFANANA
Polisi Kigoma waanza uchunguzi ukusanyaji wa vitambulisho vya kura
Hukumu rufaa kesi ya Nyundo na wenzake leo
Samia aweka shada la maua kaburini kwa Mkapa