September 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi wanaendelea kumshikiria kada wa Chadema kwa kusambaza taarifa za uzushi

 

JESHI la Polisi mkoani Morogoro, bado linaendelea kumshikilia Lucy Shayo, mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), likimtuhumu kusambaza taarifa za uwongo, uzushi na zinazoleta taharuki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro leo Jumapili, kamanda wa polisi mkoani humo, Kamishena Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Alex Mkama, amedai kuwa kukamatwa kwa Lucy, kunatokana na mwanadada huyo, kusambaza mambo mbalimbali ya uwongo na yanayoleta taharuki nchini.

Miongoni mwa aliyotaja kuwa yamesambazwa na Lucy, ni madai kuwa mabasi yanayotumiwa na Chama Cha Mapijdzo (CCM), kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Amesema, “Jeshi la polisi mkoani Morogoro, linaendelea kumshikilia Lucy Saimon Shayo (32), mkulima, mkazi wa Luaha Mbuyuni, mkoa wa Iringa na mwenzake, Steven Godwin Simshimba, mwenye umri wa miaka 41, ambaye ni mtekenolojia, mtumishi wa serikali na mkazi wa mkoa wa Tanga na kwa sasa anaishi mkoani Morogoro kwa kazi maalum.

“Kwamba, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wamepanga na kuishi kwenye chumba kimoja, kuanzi tarehe 16 Agosti mwaka huu. Hii ni kwa mujibu wa mkataba wa upangaji. Nyumba waliopanga inamilikiwa na Focas Ndungulu, mkazi wa Fokleni, Mtaa wa Mlimani.”

Anaongeza, “ukamataji umefuata sheria na taratibu. Ukamataji umeshirikisha viongozi wa mtaa wanaoishi. Watuhumiwa wamekamatwa kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uzushi na uchunguzi unaendelea, kuwatafuta watu wengine wanashirikiana nao.

“Huyu Steven Godwin Simshimba, ni mtumishi wa serikali, kama mtekenolojia wa maabara. Shughuli zake anazifanyia mkoani Tanga. Kuja kwake mkoani Morogoro, alikuja kwa wito maalum wa serikali wa kuhakiki na usahihishaji wa mitihani ya vyuo vya afya.

“Ni katika ujio huo, akamualika huyu Lucy kuja kuishi naye na wamekuwa wakiishi pamoja kwenye nyumba hiyo, tangu 22 Agosti mwaka huu.”

Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi, baada ya upelelezi kukamilika, watuhumiwa hao wawili, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

About The Author

error: Content is protected !!