
MAHAKAMA Kuu, jijini a Dar es Salaam, itaamua pingamizi la Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya Serikali, Jumatatu wiki ijayo. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu anayeshitakiwa kwa kosa la uhaini, aliwasilisha pingamizi hilo, Jumatatu wiki hii, baada ya kesi kuletwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa shitaka.
Hoja ya Lissu ni kwamba mchakato wa kukamatwa kwake na kisha kushitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumefanyika kinyume cha sheria.
Amesema, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), inaeleza wazi wazi kuwa mtuhumiwa anashitakiwa alipokamatwa. Amesema, yeye alikamatwa wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Alipaswa kushitakiwa Mbinga na siyo Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Aidha, Lissu ameiambia mahakama kuwa mchakato wa kisheria wa kuhamisha kesi kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu (Commital Proceedings), umekosewa. Ameomba majaji wa Mahakama Kuu, kuufuta na kumuachia huru.
Amesema, Mahakama ya Kisutu, imepoka haki yake ya kuita mashahidi, na kwamba nyaraka za mchakato wa kesi hiyo, zimebadilishwa kinyume cha sheria.
Mwasiasa huyo machahari nchini anasema, yote hayo yamefanyika kwa nia ovu na hivyo ameiomba Mahakama Kuu, kuufutilia mbali mchakato huo na kuamuru kuachiwa huru, ili arudi nyumbani kujumuika na familia yake.
Shauri dhidi ya Lissu, linasikilizwa na majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru. Majaji wengine, ni James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga na Job Mrema, ulipinga maombi ya Lissu. Walisema, msimamo wa kisheria hauoni kama madai hayo yana miguu ya kujisimamia.
Baada ya ubishani mkali wa kisheria uliochua siku takribani nne, Jaji Ndunguru na wenzake, waliamua leo Alhamisi, tarehe 11 Septemba 2025, kwamba Mahakama Kuu, itatoa maamuzi ya mapigamizi hayo, tarehe 15 Septemba 2025.
Mapema Lissu aliiambia mahakama iliyofurika mamia ya wanachama, viongozi na washabiki wa chama chake, kwamba hakuna sababu ya shauri hilo, kurejeshwa Kisutu wala Mbinga, ili kuanza upya comito.
“Kuna mambo makubwa yamekosewa pale Kisutu. Kuna hoja nyingi zimetolewa. Swali ni mfanyaje? Mahakama ifanye nini?
Turudi Kisutu? Hili ndio Swali lililoulizwa tangu juzi. Turudi Kisutu? Hapana. Nimesema, nirudi nyumbani kwangu nikalale na familia yangu,” alieleza
Aliongeza: “…wakati namalizia hoja yangu nilisema futeni haya mashauri niliwaambia.Kama mahakama ya kisutu haikuwa na mamlaka basi maana yake tunaendaje Kisutu? Kuna kesi gani sasa kama mmefuta comito?”
Alisema, “…waheshimiwa majaji, hii sio kesi rahisi na kufanya maamuzi ninayotaka mfanye sio maamuzi rahisi pia. Mnapaswa kufanya maamuzi bila kuogopa chochote. Msimame kwa miguu yenu. Mjiamini na mquash this proceedings (mfute mwenendo wa kesi wa Kisutu). Yaondoeni haya mashitaka.”
Akimaliza hoja zake, Lissu alisema, “Mpaka hapa tulipo mkinipeleka Mbinga naenda kufanya nini? Labda niende kumsalimia Dada yangu pale Songea na sio mimi kwenda Mbinga kushitakiwa. Mkifuta kesi siendi gerezani Ukonga. Naenda nyumbani kwahiyo majibu ya hilo swala la Mbinga ndio hilo.”
ZINAZOFANANA
Mpina ashinda kesi, mahakama yamruhusu kurudisha fomu
Takukuru yaonya wagombea wanaolipuka na ahadi za kampeni
Waliofungua kesi ya mgawanyo wa raslimali za Chadema waibua mapya