September 5, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Si aibu kubeba watu kuleta kwenye mikutano – Rais Samia

Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan

 

MGOMBEA urais, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema, siyo aibu kwa chama cha siasa, kusafirisha wanachama wake, kuhudhuria mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera zake na Ilani yake ya uchaguzi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Mbeya … (endelea).

Rais ameeleza hayo leo, tarehe 5 Septemba 2025, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni mjini Tukuyu, wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Mgombea huyo amesema, kufanya ni kuwawezesha wananchi kusikia Ilani ya CCM na miradi iliyotekelezwa, lakini hawawezi kutoa watu kwenye Wilaya moja kwenda nyingine, bali ni watu wanaotoka kwenye Wilaya husika.

“Kwakweli lazima tutoe watu. Huwezi kutegemea mtu anatoka kilomita 90 au 100 ndani ya Rungwe atembee kwa miguu hadi afike hapa,” ameeleza.

Amesema, “…lazima tuwasaidie usafiri kufika hapa, hiyo ni hakika. Lakini hatutoi watu wilaya nyingine kwenda wilaya nyingine, tunatoa ndani ya wilaya husika.”

Samia amebainisha kuwa chama chake, ni chama kinachojivunia nguvu ya wanachama wake, hivyo kuwapatia usafiri wa kuwasogeza karibu na mikutano si jambo la ajabu; bali ni kuonesha mshikamano na kuwajali wananchi.

“Kama wana imani ya kuja kusikiliza, lazima tuwape imani ya kuwasogeza kuja kusikiliza. Kwa hiyo, siyo shida wala siyo aibu kwa chama kusafirisha wanachama wake kuja kusikiliza Ilani na yale tuliyowatendea,” ameeleza Samia.

Aidha, katika mkutano huo, rais Samia amewashukuru wananchi wa Rungwe kwa kujitokeza kwa wingi, akisema hamasa hiyo inaonesha imani ya wananchi kwa chama chake.

Chama Cha Mapinduzi, kilizindua kampeni zake, jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Agosti na kutoa ahadi kadhaa za kitaifa, katika maeneo mbali mbali nchini.

Mathalani, katika eneo la afya, mgombea wa CCM aliahidi bima ya afya kwa wote; wagonjwa wa saratani, sukari na figo, kugharamiwa na Serikali.

Alisema, serikali itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000 na atapiga marufuku hospitali yoyote nchini kuzuia miili ya marehemu.

Katika kupunguza tatizo la uhaba wa ajira, Samia aliahidi kuajiri walimu 7000 na kutenga Sh. 200 bilioni, ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabishara ndogondogo.

Kuhusu mfupa wa muda mrefu wa ujio Katiba mpya, rais Samia ameahidi chama chake, kuhuisha mchakato huo na kuunda Tume ya Maridhiano na Upatanishi, itakayosaidia kuwaleta pamoja wadau wa kisiasa.

About The Author

error: Content is protected !!