
TUME ya uchaguzi nchini (INEC), imemuondoa Luhaga Mpina, katika kinyang’anyiro cha mgombea urais, katika uchaguzi mkuu ujao. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya tume, Mpina amepoteza sifa ya kuwa mgombea wa nafasi hiyo, kufuatia Msajili wa Vyama vya Siasa, kutangaza kuwa uteuzi wake, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, kutokidhi matakwa ya kikanuni.
Uamuzi wa Msajili umekuja baada ya kupokea pingamizi lililowasilishwa na anayejiita mwanachama wa ACT-Wazalendo, Monalisa Ndala.
Aidha, tume imefuta barua yake ya awali iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi na kumzuia Mpina kufika ofisi zake mjini Dodoma, huku chama chake – ACT Wazalendo – kikitarajiwa kutinga mahakamani kupinga uamuzi huo.
Tayari tume uchaguzi, imewateua wagombea wa urais kutoka vyama 16 vya siasa, kupambana katika kinyang’anyiro hicho, kilichopangwa kufanyika 29 Oktoba mwaka huu.
Uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unafanyika huku chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema), kikiwa nje, kutokana na madai kusisitiza sharti la kufanyika marekebisho kwenye mfumo wa uchaguzi, ili kuwapo na uchaguzi huru, haki na unaoaminika.
Naye mgombea wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias, ameenguliwa katika mbio za urais, kwa maelezo kuwa amekiuka taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi wa ndani ya chama.
Katika uamuzi wake aliyoufanya jana Jumanne, Jaji Francis Katabazi Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa, ameeleza kuwa Mpina hana sifa ya kugombea nafasi hiyo, kwa kuwa alipata uanachama tarehe 5 Agosti 2025, nje ya muda uliyowekwa na kanuni za chama hicho.
Alisema, kanuni za uchaguzi za ACT-Wazalendo, zinamtaka mwanachama anayetaka kugombea nafasi ndani ya chama hicho, kuwa amejiunga angalau siku saba kabla ya muda wa kutangazwa mchakato wa uchaguzi.
Msajili wa Vyama vya Siasa alitangaza jana kuwa uteuzi wa Mpina kupitia chama chake hicho kipya, haujakidhi matakwa ya kikanuni, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.
Katika uamuzi uliotolewa jana (26 Agosti), Jaji Mutungi, alibainisha kuwa Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama chake.
Amesema, mwanasiasa huyo, alijiunga ACT-Wazalendo nje ya muda uliopangwa na hivyo hakustahili kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Wataalamu wa sheria wameeleza kuwa hata kama Tume itakubaliana na maamuzi ya Msajili, mgombea huyo bado ana nafasi ya kwenda Mahakamani kuomba zuio la utekelezaji wa uamuzi wa Msajili pamoja na Tume hadi pale shauri la msingi litakaposikilizwa.
Kwa mujibu wa malalamiko ya Monalisa aliyoyawasilisha kwa Msajili, mgombea huyo alikiuka sheria ya chama cha ACT- Wazalendo, kwa kutokuwa mwanachama wa chama hicho siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.
Monalisa anasema mwisho wa kuchukua fomu za uteuzi wa mgombea urais ndani ya chama ulikuwa 25 Mei 2025, kabla ya Mpina kuwa mwanachama na hivyo kuwa nje ya muda kimchakato wa kikanuni za kiuchaguzi.
Hata hivyo, uongozi wa ACT-Wazalendo kupitia Katibu Mkuu, Ado Shaibu, umetangaza kushtushwa na uamuzi huo na kueleza kuwa tayari wameanza mchakato wa kufungua kesi Mahakama Kuu ili kupinga hatua ya Msajili, wakidai imekiuka taratibu na kuingilia mchakato wa ndani wa chama.
Kufuatia maamuzi hayo, vyama ambavyo sasa vimepitishwa kushiriki uchaguzi mkuu wa rais, katika uchaguzi wa mwaka huu, ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichomsimamisha rais Samia Suluhu Hassan; Chama Cha Wananchi (CUF) kilichomsimamisha Gombo Samandito Gombo, NCCR-Mageuzi, kilichomsimamisha Haji Ambary Khamis na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kilichomsimamisha Salum Mwalimu.
Chama cha United Democrat Party (UDP), mgombea wake, ni Saum Hussein Rashid, Tanzania Labour Party (TLP), amepitishwa Yustas Mbatina Rwamugira; chama cha Democratic Party (DP), mgombea wake, ni Abdul Juma Mluya na chama cha MAKINI, mgombea wake, ni Coaster Jimmy Kibonde.
Kwa upande wa TADEA, mgombea wake, ni Georges Gabriel Bussungu; chama cha Multiparty Democracy (UMD), mgombea aliyethibitishwa, ni Mwajuma Noty Mirambo, chama cha United People’s Democratic Party (UPDP), amepitishwa Twalib Ibrahim Kadege na National Reconstruction Alliance (NRA), aliyeteuliwa kuwania urais, ni Hassan Kisabya Almas.
ZINAZOFANANA
Mambo matano ya Mwabukusi aliyomwambia Rais Samia
Mpina ang’olewa kugombea Urais kupitia ACT Wazalendo
Musiba akimbilia ACT-Wazalendo