August 22, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tutende haki, tutavuna amani

Rais Samia Suluhu Hassan

 

KILA mwaka wa uchaguzi unapofika, wimbo mkubwa unaoimbwa kwa haraka na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kudumisha amani ya taifa. Anandika Sylvester Hanga … (endelea).

Huu ndio mtaji mkuu wa chama tawala kuhadaa wananchi, ili kiendelee kubaki madarakani na hulitamka neno hili, kila mara.

Huwezi kumsikia kiongozi wa CCM au mteuliwa wa rais, akitamka neno haki. Kama atafanya hivyo, basi itakuwa hakupitia hotuba iliyoandikiwa kabla ya kusimama jukwaani.

Hii ni kunzia mkutano wa kitaam, kidini, kijanii au kisiasa.

Tangu kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi (1995), CCM wamewakaririsha wananchi wa kipato cha chini, kwamba bila chama hicho kushika Ikulu, nchi itakumbwa na vita.

Bali hivyo siyo vita dhidi ya umaskini, maradhi, rushwa na ujinga. Ni vita vya kukiondoa chama tawala ili kuleta haki inayoweza kuleta amani ya kweli na sio maigizo.

Nguvu inayotumika kutamka neno AMANI ingetumika zaidi kwenye neno HAKI, Watanzania wasingekuwa wanaishi kwa dhiki itokanayo na ukosefu wa haki ya kuishi, kupata elimu, malazi na kutoa maoni.

Unaweza kujiuliza: Nchi inayojinasibu kuwa na Amani inawezaje kuorodheshwa kuwa miongoni mwa mataifa 10 duniani ambayo wananchi wake huishi kwa hofu na pasipo na furaha!

Inakuwaje nchi inayoimbwa na viongozi ngazi zote kuwa ni mfano wa nchi yenye amani duniani, inajikuta kwenye kundi hilo, ambalo huwapo nchi zilizokubwa misukosuko ya machafuko?

Ni kwa sababu, idadi kubwa ya viongozi wa CCM wanaimba wimbo huu mtamu kuliko wimbo wa haki wana siha njema kuliko wananchi waliowengi.

Katika kipindi hiki cha kabla na wakati wa kampeni, viongozi wachache wa vyama hasa kilicho Ikulu, hupata ukwasi wa ghafla na kukamilisha miradi yao binafsi kwa ajili ya matumbo yao.

Kwa kutumia wimbo mtamu wa amani, baadhi ya viongozi wa chama tawala na baadhi vinavyoibuka na kufadhiliwa nyakati kama hizi, huongeza idadi ya mavazi, hutanua malazi na kufuta ujinga kwa kuwasomesha watanzania somo la amani huku wakiondoka na bahasha kila baada ya vikao vyao.

Kama kuna mwana-CCM au wa chama kilichofadhiliwa “kufufuka” mwaka wa uchaguzi ambaye hajapata senti isiyo halali – asiyoitolea jasho – aungame kwa Mungu wake aliye sirini kwa kutamka kimya kimya, “simo katika kundi hilo!”

Ndio sababu baadhi ya viongozi wa chama hiki, hawataki suala la Katiba, ambalo ndiyo chimbuko la amani ya haki.

Anayetenda matendo ya haki ndani ya familia, ukoo, kitongoji, kikundi na hata nchi, anatangaza amani na haki kwa pamoja.

Anayefanya usanii, anaishia kutangaza Amani bila kutaja haki.

Katika jamii yoyote, watu huelewa neno amani kama utulivu, kimya au kutokuwepo kwa vurugu.

Hata hivyo, amani peke yake haiwezi kudumu bila haki. Haki na amani ni kama pande mbili za sarafu moja; moja ikikosekana, nyingine hubaki dhaifu, yenye doa na isiyo na maana ya kudumu.

Mtu anayefanya matendo ya haki – katika familia, ukoo, kitongoji au hata taifa – anatangaza amani yenye mashiko.

Haki inaposhuhudiwa, kila mmoja hujua nafasi yake, hujihisi salama na huona thamani ya kuendelea kushirikiana na wenzake. Hapo ndipo amani ya kweli huzaliwa.

Kwa bahati mbaya, mara nyingi au zote chama tawala nchini Tanzania, kinatangaza amani bila kutaja haki.

Kwamba, wanapoisemea amani peke yake, huwa wanazungumzia utulivu wa juu juu, kimya kinachozaliwa na woga, au kukubali mambo kwa shingo upande. Ni amani ya usanii, isiyo na uhalisia.

Katika taifa, haki ni pamoja na uwakilishi wa kweli wa wananchi, mgawanyo sawa wa rasilimali na kuheshimu misingi ya Katiba. Tutangulize haki, tutavuna Amani.

About The Author

error: Content is protected !!