August 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mpina amtumia Nyerere kujinadi urais

Luhaga Mpina, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo

 

MGOMBEA urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina ametumia jina la Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere kuomba Watanzania wamchague yeye na chama chake. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).

Mpina amesema Mwalimu Nyerere aliwahi kusema “Watanzania wanataka mabadiliko wasipoyaona au kuyapata ndani ya CCM watayatafuta nje”.

Amesema Katiba mpya na mbadiliko mbalimbali yameshindwa kufanyika kutokana na uongozi mbovu wa chama tawala kilichochoka na kinapaswa kipumzishwe.

“Nyerere alikuwa sahihi, kinachotokea hivi sasa ni aibu kwa taifa yaani imefikia mahali makanisa, misikiti inafungiwa huku viongozi wa dini wanapigwa. ACT-Wazalendo hatutakubali uonevu huu” amesema

Mwanasiasa huyo aliyehamia ACT-Wazalendo wiki iliyopita akitokea CCM alikoenguliwa kwenye mchujo wa kuwania ubunge jimbo la Kisesa, amesema ACT-Wazalendo ndiyo jukwaa sahihi la kufanya siasa za kizalendo.

Amesema kuwa baraza kivuli la mawaziri la chama hicho limekuwa likichambua ripoti mbalimbali ikiwemo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kutoa ushauri wa kinachopaswa kufanywa.

“Anayepaswa kupambana na ufisadi anawaambia mawaziri wale kwa urefu wa kamba yao, ACT-Wazalendo hatutacheka na mafisadi, watekaji na wasiowajibika”

“Nyerere aliwaambia CCM mtu anayeteuliwa kuwania uongozi ni lazima aaminike na awe na ujasiri wa kupambana na rushwa. CCM hakuna anayeweza kujitokeza mbele ya umma kusema anapambana na rushwa na akaaminika. Mimi ninao uwezo huo na wananchi wanajua” amesema.

Amesema kuwa wakiingia madarakani watafumua mfumo mbovu unaolinda maovu na kutafuna rasilimali za nchi kwa masilahi ya wachache.

“Tutawapunguzia wananchi mzigo wa kodi na kuweka mazingira bora ya watu kufanya shughuli zao kwa ufanisi. Sisi hatutakuwa na mzaha katika kupigania masilahi ya wananchi” amesema.

Amesema akiwa Rais wafanyabiashara na makundi mbalimbali hawatanyanyasika wala kuonewa kama wanavyofanyiwa na CCM.

“Nashangaa kuona hata wafanyabiashara wanaoonewa na kutolipwa fedha ndiyo wanaotoa fedha za kuichangia CCM izitumie kwenye kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 Oktoba 2025” amesema

Mpina amesema Tanzania si masikini bali rasilimali zake zinatumiwa vibaya na watawala waliojaa upendeleo, uonevu na ufisadi unaowanufaisha wachache.

“Safari hii nimeona niache kuwa mshauri (mbunge) bali niwe muamuzi (rais). Naamini ndiyo mwisho wa maisha magumu kwa Watanzania” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!