August 14, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mpina:CCM haikarabatiki ni chuma chakavu

Luhaga Mpina, Mgombea Urais wa ACT Wazalendo

 

MGOMBEA urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikarabatiki kwa kuwa kimepoteza dira na mwelekeo wake. Anaripoti Salehe Mohamed, Dar es Salaam … (endelea).

Mpina amekifananisha chama hicho tawala na gari bovu lisilokarabatika bali kuuzwa kwa kilo kama chuma chakavu.

Kauli hiyo ameitoa leo, tarehe 14 Agosti, 2025 wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu sababu za kujiunga na ACT-Wazalendo na mambo atakayofanya akichaguliwa kuwa rais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mbunge wa Kisesa kwa tiketi ya CCM kwa miaka 20 kabla ya wiki iliyopita kujiunga na ACT-Wazalendo amesema chama hicho kimekubuhu kwa uonevu, chuki, upendeleo na kutoweka mbele masilahi ya umma.

“Leo hii mafisadi ndiyo wanalindwa na CCM, chama kinashabikia watu kutekwa, kudhulumiwa, sisi na mambo yasiyofaa. Kwa hali ilivyo wananchi wenzangu tuachane na chama hiki” amesema.

Amesema kuwa CCM wamelenga kuandaa Bunge dhaifu litakalopitisha mikataba ya hovyo na litakalopigia debe kila kinachopelekwa kwao na serikali.

“Ukiangalia kwa namna wabunge machachari walivyoanguka kwenye kura za maoni unaona fika kuwa chama kimetekwa na mafisadi ambao hawataki Bunge imara la kuisimamia serikali kikamilifu” amesema

Amesema kuwa kubadilishwa mara kwa mara kwa viongozi wakubwa wa serikali na CCM ni kuonyesha kuna mambo yasiyofaa na anayewateua si mvumilivu anapokosolewa au kuambiwa ukweli.

“Watanzania ni lazima wajue kuwa sasa ni wakati mwafaka kwa CCM kupumzishwa la sivyo mambo yatakuwa mabaya zaidi siku zijazo.

” ACT-Wazalendo mkituchagua tutawaonyesha kwa vitendo namna nchi inavyopaswa kuongozwa kwa haki na kuzingatia masilahi ya wote” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!