August 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mpina hatua moja mbele mgombea urais ACT-Wazalendo

 

LUHAGA Mpina, aliyekuwa mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo la Kisesa, anatarajiwa kuwa mgombea urais wa ACT-Wazalendo, katika uchaguzi ujao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa mapema leo Jumatano, tarehe 6 Agosti inasema, kikao maalum kilichofanyika jana tarehe 5 Agosti 2025, kwenye ukumbi wa Hakainde Hichilema pamoja na mambo mengine ilipendekeza majina ya wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Urais wa Zanzibar.

Kwamba, kwa upande wa urais wa Muungano, majina yaliyopendekezwa, ni Aaron Kalikawe na Luhaga Mpina; kwa upande wa Zanzibar, anayependekezwa ni Othman Masoud Othman.

Othuman – Makamu wa Kwanza wa Rais Visiwani, ndiye mwanachama pekee wa chama hicho, aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Othman ni Mwenyekiti wa Taifa wa ACT – Wazalendo.

Majina ya wagombea yaliyopendekezwa yatawasilishwa kwa Mkutano Mkuu Taifa kwa ajili ya kupigiwa kura.

Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ilipokea na kuridhia hatua ya mgombea wa Urais wa Muungano, Dorothy Jonas Semu, kujitoa kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Semu alieleza ya chama chake, kwamba aliamua kuchukua fomu ya kugombea urais, kama sehemu ya kutekeleza majukumu yake kama Kiongozi wa chama hicho.

Alisema, “Ni wajibu wangu kukiwezesha chama changu kuingia katika mapambano ya kuiondosha CCCM madarakani kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa ya sasa.”

About The Author

error: Content is protected !!