August 2, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mawakili wa Lissu wakemea manyanyaso dhidi ya mteja wao

 

JOPO la mawakili wa Tundu Lissu, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini (Chadema), anayeshikiliwa gerezani kwa tuhuma za uhaini, wameituhumu serikali, kumtomtendea haki mteja wao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, tarehe 1 Agosti, mawakili hao wamesema, “Lissu anatendewa kama manyama” na kuongeza, “Hatupigi magoti kuomba upendeleo, hapana. Tunataka haki mbele ya uso wa mahakama.”

Akizungumza kwa hisia kali, Dk. Rugemeleza Nshalla, mmoja wa mawakili wa mwanasiasa huyo amesema, “

Dk. Nshalla alikuwa akizungumzia kitendo kilichofanywa na mmoja wa maofisa usalama aliyevalia sare za jeshi la Magereza, aliyemsukuma Lissu hadi kutaka kumuangusha, akiwa mahakamani Jumanne wiki hii.

Amesema, “…kitendo hicho, ni kinyume na Katiba na Haki za binaadamu. Ni kinyume na sheria zinazoongoza jeshi la magereza na kinyume na kwamba mengi anayofanyiwa Lissu, ni kinyume cha taratibu za kuendesha kesi mahakamani.”

Aidha, Dk. Nshalla amesema, sio sahihi kwa askari magereza kujificha sura zao kwa kuwa hayo ni maandalizi ya kufanya matendo yenye nia ovu.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Nshala amesema, wamemuandika barua Jaji Mkuu, George Mcheche Masaju, kumtaarifu yanayoendelea kwenye mhimili huo wa Mahakama.

“Lengo la barua hii, siyo kuomba upendeleo. Ni kukemea na kuzuia matendo yanayokinzana na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” ameeleza Dk. Nshalla.

Ametaka askari aliyefanya kitendo hicho atafutwe na awajibishwe kwa mujibu wa kanuni za Magereza.

Naye Mpale Mpoki, wakili mwingine wa Lissu, amesema kuwa hakuna aliye juu ya sheria na kwamba, “Kila mtu akifuata sheria katika kesi hii, itaonekana haki imetendeka.”

Amesema, askari magereza wametenda matendo ya kuutweza utu wa Lissu.

“Vitendo vinavyofanywa na askari magereza visizidi mamlaka ambayo wamepewa na sheria au na Katiba.

“Katiba yetu, inakataza kumtesa mtu, kutweza utu wake na kwa hiyo kumsukuma mtu ni kutweza hadhi ya mtu ambaye yupo mahakamani,” ameeleza.

Amesema, mahabusu anastahili haki zote haki pekee anayokosa ni kwenda anapotaka. “Lissu hajapatikana na hatia, hivyo anapaswa kutendewa kama mtuhumiwa,” amefafanua.

Wakili huyo, alitoa kauli hiyo, wakati akijibu maswali ya mwandishi wa habari, waliotaka kufahamu hatua ambayo mawakili hao wanachukua na tafsiri ya kitendo kilichofanywa na afisa huyo wa magereza.

Katika oucha za cideo zilizosambaa mitandaoni, afisa huyo wa magereza ameonekana akimsukuma kwa nguvu mshitakiwa huyo ambaye ni mlemavu wa mguu, uliyotokana na shambulio la risasi alilofanyiwa Septemba 2017.

Kesi ya uhaini ambayo Lissu anashitakiwa na Jamhauri, akipatikana na hatia, hukumu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Mbali na kesi hiyo, Lissu anashitakiwa kwa kosa jingine la kuchapisha taarifa za uongo. Katika kesi hii, akipatikana na hatia aweza kutozwa faini au kufungwa kuanzia miaka mitatu au yote mawili.

Lissu alikamatwa na kufunguliwa mashitaka hayo, miezi mitatu baada ya kumuangusha aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema kwa muda wa miaka 21, Freeman Mbowe, katika uchaguzi huru, wazi na haki.

Tangu kuangushwa kwenye uchaguzi huo, tarehe 21 Januari mwaka huu, Mbowe amejitenga na shughuli za Chadema; hajaonekana mahakamani wala hajakemea anayotendewa mwenyekiti wake.

Lissu alikuwa mmoja wa watetezi wakubwa wa Mbowe katika tuhuma zote zilizokuwa zikimkabili wakati akiwa mwenyekiti wa chama hicho.

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, wanahusisha moja kwa moja na kesi alizofunguliwa Lissu na anguko la Mbowe.

Tayari baadhi ya wafuasi wake, wakiwamo waliokuwa manaibu makatibu wakuu wa Chadema – Bara na Visiwani, wamejiengua ndani ya chama hicho na kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wanakotuhumiwa kutumikia serikali, kudhoofisha Chadema na kumkandia Lissu.

Lissu aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Rais wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na mwanaharakati mahiri nchini, amefanya kazi kubwa nchini zinazoendelea kukuza jina lake katika siasa.

About The Author

error: Content is protected !!