July 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Zanzibar yatajwa kughairishwa Kamati Kuu CCM

Amos Makala, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM

 

KIKAO cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichopangwa kufanyika leo jijini Dodoma, kimeripotiwa kughairishwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, kughairishwa kwa mkutano huo, “kumetokana na mambo kuvurugika Visiwani Zanzibar.”

Mkutano wa leo wa Kamati Kuu, ulikuwa mahususi kupitisha majina ya wanachama wa chama hicho, waliomba kuteuliwa kuwa wagombea wa ubunge katika Bunge la Muungano na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Hata hivyo, gazeti hili halijaweza kupata kwa undani kilichotokea Zanzibar.

Mmoja wa watoa taarifa wetu ameishi kusema, “Kule Visiwani kunawaka moto. Viongozi wanatarajiwa kwenda huko leo jioni.”

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za CCM, Kamati Kuu, ina wajibu wa kupitisha majina matatu ya wanachama waliomba kugombea ubunge na ujumbe baraza, ili kupigiwa kura na viongozi wa mashinani.

Matokeo ya kura hizo za maoni, zitatumika kukisaidia chama kupitisha jina moja la mgombea katika kila jimbo la uchaguzi.

MwanaHALISI Online limeelezwa na vyanzo vyake vya kuaminika kutoka ndani ya CCM kuwa kikao cha Kamati ya Maadili na Usalama, kilichotarajiwa kufanyika jana tarehe 18 Julai, hakikuweza kufanyika.

“Kikao cha Kamati ya Maadili, kilichopangwa kufanyika jana Ijumaa, hakikuweza kufanyika. Hivyo, kikao cha CC kilichopangwa kuwapo leo 19 Julai 2025, nacho hakiwezi kufanyika,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho, kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Gazeti hili limeshindwa kumpata msemaji wa chama kilichopo madarakani, kuzungumzia suala hilo. Tutaendelea kumtafuta.

Maamuzi ya mwisho ya uteuzi wa wagombea ubunge wa jimbo na ujumbe wa baraza la wawakilishi, pamoja na wale wa viti maalum, ikiwamo kupitia makundi mbalimbali – Baraza na Visiwani – yatafanywa na Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya chama hicho.

Kuahirishwa kwa vikao hivi kunakuja wakati ambao wagombea mbalimbali wa chama hicho, wakiwa na presha ya kujua hatma yao, kuelekea mchakato wa ndani wa uteuzi.

About The Author

error: Content is protected !!