
NIKISEMA mbio za Pande Marathon hazijapata kutokea, nina maanisha. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwenye uzinduzi wa msimu wa kwanza wa Msakuzi Pande Marathon ambazo mbio zake zilifanyika mwishoni mwa wiki ndani ya Msitu wa Pande, uliopo Ubungo, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Waandaji wa mbio hizo, Msakuzi Sports Promotion, wakiongozwa na Mwenyekiti wao Dk. John Kisimbi, ndio waliofanikisha msimu wa kwanza wa mbio hizo kwa viwango vya juu vya ubora.
Mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Makumbusho na Utalii, Dk. Noel Luoga ambaye alimwakilisha Waziri wa Maliasi na Utalii, Dk. Pindi Chana.
Katika mbio hizo, washindi wa kilomita 21 upande wa wanaume walikuwa Jonas John, mkazi wa Singida, Imradi Gad na Jamali Said, wote mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Wanawake wa kilomita 21, washindi ni pamoja na Glory Silvester, Debora Benedictor na Witnes Mhinjo, wote wakazi wa Dar es Salaam.
Washindi wa kilomita kumi, upande wa wanawake ni Irine Dumba, Glory Mushin na Brigita Isdori wa jijini Dar es Salaam.
Upande wa wanaume washindi walikuwa ni Mussa Ramadhani, Harid Chambili na Nickson Swai. Washindi wote walipata zawadi nono na medali.
Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) ambao waliridhia mbio hizo kwa mara ya kwanza kufanyika ndani ya Msitu Pande, wanakiri kuwa kusanyiko la washiriki wa mbio hizo, halijapata kutokea ndani ya hifadhi hiyo.
Tofauti ya mbio za Pande Marathon na zingine ni kwamba nyingi zinafanyika kwenye barabara nzuri za lami, kwenye viwanja kama vya mpira, lakini hizi zilikuwa msitu kwa msitu, pori kwa pori.
Washiriki walikuwa wanakimbia huku wakifurahia kuona uoto wa asili na kupishana na wanyama wanaovutia ndani hifadhi hiyo.
Baadhi ya njia walizokuwa wanakimbia, kwa juu zimefunikwa na msitu mnene kiasi cha kushindwa kuona jua.
Baadhi ya washiriki waliliambia Gazeti hili kuwa moja ya vitu vya kuvutia kwao mbali ya kuona wanyama ilikuwa uoto wa asili, hewa safi ya ubaridi ambayo iliwafanya wakimbiaji wasichoke wala kutoka jasho.
Washiriki walikuwa wanakimbia, wakikutana na wanyama, wanasimama kidogo, wanapiga nao selfii, kisha wanaendelea na mbio.
Kwa kifupi, itoshe kusema Pande Marathoni zilikuwa ni ‘Mbio, Utalii na Bata la nguvu.
Nikisema ilikuwa ni bata la nguvu maana yake ni kwamba sio tu kwamba walikimbia, bali pia washiriki walifanya utalii wa kuona wanyama, lakini mwisho wa siku walipata nyama choma ya pori na kuselebuka na muziki wa dansi ulioporomoshwa na bendi ya Acudo Sound.
Katibu wa Msakuzi Sports Promotion, Dk. Emmanuel Nundu, Mratibu Mkuu, Filbert Mosha, Peter Nkulila, Chester Kapinga na wengine kwa nyakati tofauti wameahidi kufanya maboresho ili mbio hizo mwakani zifikie viwango vya kimataifa
Dk. Kisimbi alisema huo ni mwanzo tu kwani mwakani mbio hizo zitaboreshwa na zitajumuisha washiriki wengi hasa baada ya mafanikio waliyopata katika msimu huu wa kwanza.
Idadi ya washiriki walijitokeza kutoka maeneo mbalimbali ya jijini la Dar es Salaam na nje ya mkoa huo ilikuwa ni kubwa kiasi kwamba uongozi wa TAWA ulikiri kwamba haujawahi kupata kusanyiko kubwa wa mara moja kama wa Pande Marathon.
Zilikuwa ni mbio za aina yake, washiriki ambao walianza mbio hizo saa moja na nusu asubuhi, walikuwa na njia tofauti na kupitia hadi kwenye kilele cha hitimisho.
Mosha anaungana na Dk. Kisimbi kwa kuweka msisitizo kuwa msimu ujao wa Pande Marathon, sio wa kukosa kwani changamoto zote zilizojitokeza, zitazibwa mwakani.
Changamoto kubwa inayoonekana ni barabara ya kufika katika hifadhi hiyo ya taifa
Baadhi ya washiriki wameiangukia Serikali kutengeneza barabara iendayo kwenye msitu huo kwa kiwango cha lami ili kuvutia wengi na kuongeza pato la taifa kupitia utalii.
“Barabara niliyopita hadi kufika hapa na mambo niliyoshuhudia, nimebaki najiuliza barabara kutoka Mbezi ya Magufuli, kuanzia pale Mbezi High hadi Msitu wa Pande kwanini isijengwe kwa kiwango cha lami,” alihoji mshiriki Gabriel Mushi.
Mshiriki huyo alisema endapo barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami na Pande Marathon ikaendelea kufanyika kila mwaka, hifadhi hiyo itakuwa inapata wageni wengi na hivyo kuungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza na kukuza utalii na vivutio vya nchi.
ZINAZOFANANA
Bashiri na Meridianbet mechi za Europa na Conference leo
NBC yakabidhi ‘Kits’ za NBC Dodoma Marathon kwa GSM Group
NBC yazitambulisha jezi za NBC Dodoma Marathon kwa wadau, Sanlam wapongeza ubora