
MFANYABIASHARA na mwanasiasa mashuhuri nchini, Rostam Aziz amedai kuwa sekta binafsi Tanzania iko tayari kusaidia kuiongoza nchi kuelekea kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akihutubia mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine waandamizi, wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya 2050 jijini Dodoma, Rostam, alisifu ushirikishwaji uliofanyika katika kuandaa dira hiyo na akaahidi ushirikiano wa sekta binafsi katika utekelezaji wake.
Rostam alisisitiza mchango muhimu wa sekta binafsi katika kuchangia maandalizi ya Dira 2050, akieleza kuwa makadirio ya awali ya pato la taifa kati ya dola bilioni 500 hadi 700 yaliongezwa baada ya hoja zenye uzito kutoka kwa viongozi wa biashara.
“Tunaamini nchi hii inaweza kuvuka dola trilioni moja. Hicho ndicho kiwango cha ndoto na matarajio ambacho Tanzania inastahili,” alieleza.
Alitoa wito wa kuanzishwa mara moja kwa Mfuko wa Kuendeleza Vipaji (Talent Development Fund), wenye thamani ya dola 70 milioni kila mwaka kwa ajili ya kufadhili mafunzo ya vijana 1,000 wenye vipaji vya kipekee kutoka Tanzania katika fani muhimu kama uhandisi, akili bandia (AI), fedha, na sayansi ya data.
Vijana hawa wangetumwa kusoma katika vyuo vikuu bora duniani na kurejea nchini kutoa huduma kwa mujibu wa mikataba ya kurejesha maarifa (bonded contracts).
Aidha, Rostam alisema kuna umuhimu wa kufanya mageuzi ya haraka katika taasisi za ndani ya nchi, akihimiza kuimarishwa kwa vyuo vikuu vya ndani, kuboreshwa kwa mitaala, na kukuza viongozi wa kizalendo ili kuendana na ushindani wa uchumi wa dunia.
“Tusisubiri tu vijana warejee kutoka nje, ni lazima tuchukue hatua sasa kujenga wataalamu wa kiwango cha dunia hapa nyumbani,” alisema.
Akitaja sekta ya viwanda kuwa nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini, Rostam aliiomba serikali kuweka sera zitakazolinda na kuzipa kipaumbele sekta za ndani. “Hakuna nchi iliyofanikiwa kujenga uchumi wa viwanda bila kutetea viwanda vyake yenyewe,” ameeleza.
Aidha, Rostam alipendekeza ubalozi wa Tanzania nje ya nchi kuwa na jukumu la makusudi katika kutambua na kuhamasisha wataalamu wa Kitanzania walioko ughaibuni kurudi nyumbani, hasa wale waliopo kwenye sekta bunifu. Alimpongeza Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmood Thabit, kwa kusimamia diplomasia ya kiuchumi na kutumia vipaji vya kimataifa kwa maendeleo ya taifa.
Akinukuu kauli ya marehemu Deng Xiaoping, kiongozi wa mageuzi ya China, Rostam aliwakumbusha waliohudhuria kuwa “amani na utulivu ni msingi wa maendeleo yote.” Alisisitiza kuwa taasisi imara, sera wazi, na uongozi wa maono ni mambo muhimu katika kufanikisha Dira 2050 na kuhakikisha mabadiliko ya muda mrefu ya nchi yanadumu.
Akizungumzia sekta ya fedha, Rostam alikosoa mifumo ya sasa ya kibenki kuwa ni migumu na haitoi mitaji ya kutosha kwa wajasiriamali wa Kitanzania kuweza kukua. “Lazima tubadili mfumo wetu wa kifedha. Hakuna biashara ya ndani inayoweza kustawi chini ya masharti ya sasa ya mikopo,” alionya.
Alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake wa nidhamu katika miaka minne iliyopita, hasa katika nyanja ya maendeleo ya miundombinu. Alimsifu kwa kukamilisha miradi ya kimkakati, kuanzisha mingine mipya, na kujenga utamaduni uendelevu wa utawala, mambo aliyosema ya kimtazamo kwa uongozi wa taifa.
“Huu ndio wakati wetu wa kusonga mbele kwa ujasiri. Tume ya Mipango lazima iwe moyo wa mageuzi haya. Sisi, sekta binafsi, tuko tayari,” alifafanua.
ZINAZOFANANA
Mohamed Abdulrahman: Gwiji la utangazaji DW laanguka
Kwaheri Joshua Nassari, Karibu DC Lawuo
Viongozi wa Chadema waachiwa kwa dhamana