July 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Sita wadaiwa kumuua Sheikh Jabir

Jabir Haidar Jabir

WATU sita wanaotajwa kuwa ni wakaazi wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar wamefikishwa mahkamani wakituhumiwa kumuua kwa makusudi mwanadini Jabir Haidar Jabir, ambaye kifo chake kilizusha mjadala mkubwa kwa vile kilivyotokea. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Sheikh Jabir alikutwa msituni eneo la Bumbwisudi, Wilaya ya Magharibi A, akiwa amefariki dunia huku vespa yake ikiwa kando ya mwili wake. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati huo na Idhaa ya Redio ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar {ZBC}, mwili wa Sheikh Jabir, aliyekuwa na umri wa miaka 56, ulikutwa usiku wa tarehe 27 Mei mwaka huu, ikielezwa kuwa alichukuliwa nyumbani kwake mtaa wa Mambosasa, Wilaya ya Magharibi B, mnamo saa 1 usiku siku hiyo.

Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Anuwar Saaduni, akisoma maelezo ya mashtaka mbele ya Jaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Khadija Shamte Mzee, Ijumaa wiki iliyopita, aliwataja watuhumiwa hao, umri wao ukiwa kwenye mabano, kuwa ni Salum Manja Ame {23}; Idrisa Kijazi Kasim {41}; Ali Mohamed Ali {30}; Ali Machano Haji {52}; Zahor Khamis Ali {54} na Mohamed Hassan Jongo {38}.

Manasheria Saaduni aliiambia Mahkama kwamba watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua kwa makusudi Sheikh Jabir, kinyume na Sheria ya Adhabu Nam 6 ya mwaka 2018, Kifungu cha 179 na 180, eneo la Kizimbani, Wilaya ya Magharibi A, majira ya Saa 3 usiku.

Taarifa ya Idara ya Uhusiano ya Mahkama Kuu Zanzibar iliyotolewa juzi imesema watuhumiwa walikana kosa na kesi kuakhiriwa hadi tarehe 16 Julai 2025 itakapofikishwa kwa kutajwa. Watuhumiwa wamerudishwa rumande.

Jaji Shamte aliakhirisha kesi baada ya Wakili Juma Kumba anayewatetea watuhumiwa kupinga kauli ya Mwanasheria Saaduni kuwa upepelezi haujakamilika. “Mwanasheria anaomba kesi kuakhirishwa kwa kuwa hawajakamilisha upelelezi wakati wateja wangu wanaendelea kukaa rumande tangu pale walipokamatwa tarehe 28 Mei, inakuaje upelelezi haujakamilika,” alilalamika.

Sheikh Jabir alikuwa miongoni mwa maulamaa wa Kiislam anayefahamika kwa kufanya kazi za kusaidia jamii hususan za maeneo ya vijijini na makundi ya watu maalum wenye hali dhalili. Kupitia vyanzo mbalimbali, akifikisha kwa wahitaji hao misaada ya chakula, nguo na fedha taslim.

About The Author

error: Content is protected !!