
Emmanuel Ntobi
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimedai kuwa wataenda mahakamani kuifungulia kesi serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupinga kufungiwa kwa mitandao ya kijamii ya ‘X’ (zamani Twitter), Clubhouse, na Telegram. Anaripoti Joyce Ndeki, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa tarehe 25 Juni 2025, na Emmanuel Ntobi- Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA ambapo amesema hatua ya serikali kuvifungia vyanzo hivyo vya taarifa ni kinyume cha Katiba ya Tanzania na inalenga kudhibiti uhuru wa taarifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, mitandao hiyo haipaswi kudhibitiwa kwa kigezo cha maudhui, ilhali taasisi na wizara za serikali zinaendelea kutumia mitandao hiyo kuweka taarifa zao.
“Inashangaza wakati Serikali inafungia mtandao wa X kwa kisingizio kuwa inachapisha maudhui ya ngono, bado Ukurasa wa Ikulu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jeshi la Polisi, vyombo muhimu vya habari vinaendelea kuweka taarifa zake kwenye mtandao huo,” amesema Ntobi.
Chama hicho kinasema kuwa kufungiwa kwa mitandao hiyo kunakiuka Ibara ya 18(1) na (2) ya Katiba ya Tanzania, inayolinda haki ya uhuru wa kutoa maoni, kutafuta na kupata taarifa bila kuingiliwa.
ACT Wazalendo pia wameonya kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kisiasa wa kudhibiti taarifa na kupunguza ushiriki wa wananchi katika mijadala ya kitaifa kuelekea uchaguzi.
Chama hicho kimetaka mitandao hiyo ifunguliwe, huku kikiweka wazi kuwa haki za kidijiti ni sehemu ya haki za msingi za binadamu ambazo serikali inapaswa kuziheshimu.
“Mitandao ya kijamii sasa sio tu ni sehemu ya kuvinjari bali ni jukwaa linalosaidia watu kujiajiri na kufanya biashara mbalimbali,” taarifa hiyo imeongeza.
ZINAZOFANANA
Kesi dhidi ya Chadema yapigwa kalenda
Janeth Rithe aachiwa kwa dhamana
ACT Wazalendo: Deni la Taifa linakuwa kwa kasi, uchumi wa nchi hatarini