May 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yaweka mikakati ya kudhibiti magugumaji Victoria

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa

 

KASSIM Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania, amesema kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea katika maeneo hayo. Anaripoti Joyce Ndeki, Mwanza … (endelea).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 19 Mei 2025, wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

”Ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji ndani ya ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea.”

Waziri Mkuu, Majaliwa amesema magugumaji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.

Aidha,amewashukuru wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugumaji hayo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.

Kwa upande wake, Cyprian Luhemeja, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira akitoa taarifa kuhusu shughuli ya kuteketeza magugumaji hayo kwa Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuyaondoa magugumaji ya asili ambayo yamesambaa katika eneo la ukubwa wa ekari zaidi ya 300.

Amesema magugumaji hayo ambayo yamegawanyika katika aina tatu (salivinia molesta ambalo ni jipya, water hyacinth na gugumaji la asili aina ya Lutende) yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya Ziwa Victoria

Katibu Mkuu huyo amesema wanatarajia kumaliza kazi ya kuyateketeza magugumaji mwezi Julai, 2025 na hivyo kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea katika ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali.

About The Author

error: Content is protected !!