May 12, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wachimbaji Geita wampongeza Rais Samia

WACHIMBAJI na wafanyabiashara wa madini wa mkoa wa Geita, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake. Anaripoti Joyce Ndeki, Geita … (endelea).

Hayo yamesemwa jana kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wachimbaji hao katika eneo la mnada wa zamani Katoro,Geita kwa lengo la kumpongeza Rais Samia kwa mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya madini.

Akitoa maelezo ya awali, Titus Kabuo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita (GEREMA), amesema dhumuni kubwa la kusanyiko hilo ni kumpongeza Rais Samia kwa kuiboresha sekta ya madini na kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na ufanyaji biashara hali inayopelekea kukua kwa shughuli za uchimbaji na kuathiri chanya maendeleo ya wachimbaji na uchumi wa nchi.

Naye John Bina, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA),  amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia sekta ya madini imeshuhudia mabadilko makubwa hasa katika upatikanaji wa Leseni kwa wachimbaji na hatua iliyoanzwa na serikali ya kufanya utafiti wa kina ili kuwaongoza vyema wachimbaji madini nchini.

Anthony Mavunde, Waziri wa Madini

Akiwasilisha hotuba yake, Anthony Mavunde, Waziri wa Madini ameyataja mafanikio 16 ya Rais Samia katika kuipaisha sekta ya madini kubwa ikiwa ni kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kufikia 10.1%,ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu, kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kuelekea lengo la kukusanya Sh. 1 trilioni na upatikanaji wa mitambo ya kuchoronga 15 kwa ajili yaa wachimbaji wadogo.

Aidha, Mavunde ametumia fursa hiyo kukipandisha hadhi kituo cha ununuzi wa dhahabu cha Katoro na kuwa soko kamili la Dhahabu la Katoro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Joseph Msukuma na Tumaini Magesa wamempongeza Rais Samia kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara ambayo yamesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa na kukuza uchumi wa watu wa Geita.

Martin R. Shigela, Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema Mkoa wa Geita umejipanga kuchochea shughuli za madini kwa kuboresha mazingira ya uchimbaji ili kukuza uchumi wa  wananchi wa mkoa wa huo kupitia upatikanaji wa leseni zaidi ya 5,308 na mitambo ya uchorongaji ambayo Rais ameitoa kwa kwa wachimbaji wadogo.

About The Author

error: Content is protected !!