May 9, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali kuongeza thamani ya madini

 

SERIKALI ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuelekea mageuzi katika Sekta ya Madini kwa kuanza mkakati wa kuongeza thamani ya madini muhimu yanayopatikana nchini. Anaripoti Joyce Ndeki, Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa na Anthony Mavunde, Waziri wa Madini jana tarehe 8 Mei 2025, wakati akizindua rasmi Taarifa ya Uchambuzi wa Kina wa Uongezaji Thamani Madini Muhimu na Mkakati ya Tanzania (Manufacturing Africa – Critical Minerals Value Addition Study), katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma

Akizungumza katika Mkutano huo uliohudhuriwa na Marianne Young, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania akiongozana na maafisa wandamizi wa Ubalozi huo, wadau wa Sekta ya Madini, Wawekezaji, na wawakilishi, Waziri Mavunde alisema kuwa utafiti huo ni hatua muhimu katika kufanikisha azma ya Taifa ya kuyachakata madini muhimu na mkakati ndani ya nchi hadi kufikia bidhaa za mwisho kwa matumizi ya ndani na nje.

“Ni maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka Mkakati kuyaongeza thamani madini muhimu yanayopatikana nchini hapa hapa ndani ya nchi. Dhamira ni kuyatumia madini yetu kama nyenzo ya kujenga uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na teknolojia,” alisema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde alisisitiza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini muhimu kama vile nickel, graphite, rare earth elements, na lithium, madini ambayo ni mhimili wa teknolojia za kisasa, magari ya umeme, na nishati mbadala duniani.

“Kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa madini haya, tunajipanga kuwa kitovu cha uzalishaji wa malighafi ya kisasa kwa ajili ya soko la kimataifa,” amesisitiza Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa, Serikali imeweka mazingira rafiki kwa uwekezaji kwa kuboresha miundombinu, kujenga uwezo wa kitaalamu, na kuweka sera na motisha zinazowezesha uwekezaji katika mitambo ya uchenjuaji, uchenjuzi, na uzalishaji wa bidhaa za mwisho.

“Utafiti huu pia utaisaidia Serikali kutambua maeneo mahsusi ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, pamoja na fursa mpya za kiuchumi zitakazochochea maendeleo hapa nchini” ameongeza Mavunde.

Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini Marianne Young alisema kuwa taarifa hiyo ni sehemu ya ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili (Tanzania na Uingereza) katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya Madini ambao pia ameeleza Mkakati wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Uingereza kushirikiana na GST kubadilishana uzoefu katika eneo la utafiti wa kina wa madini.

Uchambuzi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa ushirikiano wa kimkakati wa Ushirikiano wa Ustawi wa Pamoja (Mutual Prosperity Partnership – MPP) kati ya Tanzania na Uingereza uliozinduliwa mwaka jana. Mpango huo pia unalenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kwenye Sekta ya Viwanda, hasa kwa kutumia madini muhimu/mkakati kama malighafi ya msingi.

About The Author

error: Content is protected !!