
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja
KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kuwa na umoja wenye sauti moja yenye nguvu ili kuwa na sauti moja katika mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi. Anaripoti Joyce Ndeki, Zanzibar … (endelea).
Ametoa wito huo wakati akifunga Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) tarehe 30 Aprili 2025, uliofanyika Zanzibar ambapo amesema Afrika iliyounganishwa yenye sauti thabiti itatoa nafasi kubwa ya kuwasilisha vipaumbele vyake kwenye mikutano ya kimataifa.
Mkutano huo wa siku tatu, umewakutanisha washiriki kutoka nchi 54 barani Afrika ambao pamoja na masuala mbalimbali wamejadili ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira.
Amesema Afrika inahitaji kwenda mbali zaidi katika kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa, na kwa hivyo, tunapaswa kwenda pamoja kukabiliana na changamoto hiyo.
Mhandisi Luhemeja alisema Afrika si bara maskini, hivyo ipo haja ya kuwa na sera na mikakati inayolinda utajiri wa Afrika kwa maendeleo endelevu ya bara hilo.
Pia, Katibu Mkuu alisema kwa kuwa Afrika ndiyo iliyoathiriwa zaidi, hivyo kipaumbele cha bara ni kuwa na fedha za uhakika kwa kuzingatia vipaumbele na maslahi mapana ya watu wa barani humo.
Alisisitiza mfumo wa ruzuku ni muhimu ili kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo Afrika lazima ihamasishe upatikanaji wa Dola za Marekani 1.3 trilioni kufikia mwaka 2025.
Halikadhalika, Mhandisi Luhemeja alisema mkutano huu umesisitiza haja ya kuwa na ufafanuzi wa kupata fedha kutoka kwa Mfuko wa Hasara na Uharibifu, mchakato unaopaswa kurahisishwa kupata fedha hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Richard Muyungi alisema miongoni mwa mijadala iliyojadiliwa ni utafutaji wa kiasi cha Sh. 300 bilioni kwa ajili nishati safi barani Afrika ambayo ni utekelezaji wa maelekezo hayo ya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Alisema suala la kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa ajili ya watu milioni 300 wa Afrika kupata nishati safi lilikuwa ajenda kuu ya mkutano huo kuelekea Mkutano wa 30 Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabiachi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Belém, Brazil.
Alisema Dk. Muyungi. “Kama unavyofahamu sisi Tanzania ni mwenyekiti wa AGN kwa mwaka mzima ambapo kamati hii ilielekezwa tuwe na Sekretarieti ya kudumu ambayo itakuwa na makao makuu pake Addis Ababa nchini Ethiopia na sisi tumeahidi kabla ya mwezi Juni tutaunda kamati ya kusimamia mchakato huo,”
Dk. Muyungi ambaye pia ni Mshauri wa Rais kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira aliongeza kuwa imeazimiwa kuwa Afrika itaendelea kushirikisha,kufundisha na kujenga uwezo wa vijana kupitia kliniki za mabadiliko ya tabianchi kuhakikisha inarithisha ujuzi kwa vizazi kutetea maslahi ya Afrika katika majadiliano ya kimataifa.
Mkutano huo ulifunguliwa tarehe 28 Aprili 2025 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango.
ZINAZOFANANA
Padre Kitima amuibua Mbatia
Serikali yawaongezea mshahara wafanyakazi
Mtu mmoja mbaroni kwa kushambuliwa Padri Kitima