April 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yajivunia mafanikio sita ya TASAF

Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene

 

SERIKALI ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi Rais Samia Suluhu Hassan imejivunia uwepo wa mafanikio makubwa ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea),

Mafanikio hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka 4 ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nne kwa waandoshi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Doodoma.

Simbachawene amesema kuwa kwa kipindi cha miaka 4 ya Rais wa sasa imeoonesha mafabikio makubwa kwa upande wa Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF).

Ameyataja mafanikio hayo na kueleza kuwa ni pamoja na mpango wa Miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa na
hadi kufikia Desemba, 2024, jumla ya miradi 27,863 ya kutoa ajira za muda kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imetekelezwa ambapo jumla ya Kaya za walengwa 662,000 zimelipwa jumla ya shilingi bilioni 213.8.

Ameeleza kwamba licha ya kuongeza kipato kwa walengwa pia wameweza kupata ujuzi wa utekelezaji wa miradi hiyo unaoweza kutumika katika shughuli za kukuza uchumi wa kaya na kuongeza kipato. Miradi hii imenufaisha sekta za kilimo, barabara, misitu, maji na mazingira.

Ameelezea mafanikio mengine ni pamoja na miradi ya kuendeleza na kuboresha Miundombinu ya huduma za Jamii Jumla ya miradi 137 ya uendelezaji miundombinu yenye thamani ya Sh. 12.67 bilioni ilitekelezwa katika Mamlaka za maeneo ya utekelezaji 29.

Amesema kuwa kati ya miradi hiyo miradi 6 imekamilika na 72 ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Miradi ya aina hii imetatua changamoto za jamii zinazotokana na upungufu au kutokuwepo kabisa kwa miundombinu ya kutosha ya kutolea huduma za jamii katika sekta za Elimu, Afya na Maji.

“Miradi ya Kupunguza Umaskini Tanzania-Awamu ya Nne (TPRP IV) Hadi kufikia Desemba, 2024, jumla ya miradi ya jamii 1,518 yenye thamani ya shilingi bilioni 81.8 imetekelezwa ambapo miradi 659 imekamilika na inatumika kutoa huduma na miradi 859 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

” Idadi ya miradi hiyo kisekta ni Elimu 495, Afya 262, Barabara za Vijijini 120, Maji 23, Kilimo 11, Mazingira 6, Majosho 4 na Miradi ya kuongeza kipato 597,” ameeleza Simbachawene.

Akiendelea kuelezea mafanikio kupitia TASAF amesema kuwa Miradi ya Kuondoa umaskini awamu ya Nne (TPRP) ni mradi unaotekelezwa na TASAF kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC) katika mikoa mitano (5) ya Arusha, Geita, Mwanza, Njombe na Simiyu.

Ametaja mafanikio mengine ya TASAF kuwa ni pamoja na mpango wa kutoa Mafunzo ya Stadi za Msingi za Kiuchumi na Ruzuku ya uzalishaji kwa walengwa TASAF imetoa mafunzo ya stadi za msingi za shughuli za kiuchumi za ruzuku ya uzalishaji kwa kaya za walengwa zilizokidhi vigezo.

Sembachawene ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2024, walengwa 94,520 kwenye Mamlaka na maeneo ya utekelezaji 69 walikuwa wamepewa ruzuku ya uzalishaji ya kiasi cha shilingi bilioni 35.9 kama mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi waliyokuwa wamebuni.

Aidha ameeleza kuwa TASAF imefanikisha kujenga Rasilimaliwatu ili kujenga rasilimaliwatu endelevu yenye tija kwa ujenzi wa taifa la kesho, Mpango umeweka masharti yanayoendana na utoaji ruzuku kwa kaya za walengwa.

“Masharti hayo ni kuhakikisha kaya zenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupelekwa kliniki ili wapate chanjo muhimu na wazazi waelimishwe kuhusu lishe na vivyo hivyo watoto kuwa na afya bora.

“Kadhalika, TASAF inahamasisha kaya zenye watoto walio katika umri wa kwenda shule kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo kwa asilimia zaidi ya asilimia 80 ya siku za masomo kwa mwezi.

“Hii imesaidia watoto wengi kutoka kaya maskini kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma, kufaulu na kufanikiwa kuingia katika vyuo vya elimu ya juu.

“Aidha, TASAF kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imewezesha waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka kaya za walengwa kutambulika, kupatiwa mikopo ya elimu kwa asilimia 100. Hadi kufikia Novemba 2024 jumla ya wanafunzi 8,274 wamenufaika na mikopo hii,” amebainisha Simbachawene.

Akimalizia na mafanikio 6 kupitia TASAF kwa kipindi cha miaka 4 Simbachawene amesema kuwa kummekuwepo na kuboreka kwa hali ya walengwa katika utekelezaji wa afua mbalimbali, TASAF imefanikiwa kuhitimisha kaya za walengwa takribani 400,000 nchi nzima.

Amesema kuwa kaya hizo baada ya kuhudumiwa na Mpango kwa takribani miaka 10, zimeboresha maisha, kuongeza rasilimali na zinaweza kuendelea kuendesha maisha yao bila ruzuku ya TASAF.

About The Author

error: Content is protected !!