
Othman Masoud Othman
MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema wanaingia kwenye uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu wakiamini wao ni washindi katika uchaguzi huo kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Othman ameyasema hayo leo tarehe 16 April 2025, wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini Unguja mara baada ya kumaliza kurejesha fomu ya kugombea Urais kupitia chama hicho.
Amesema nafasi ya Uraisi kwao ipo wazi baada ya Wazanzibari walio wengi kusalitiwa kimaendeleo na kufutika kabisa matarajio yao.
Amesema Zanzibar ina nafasi kubwa ya kupiga hatua zaidi za kimaendelea iwapo kutakuwa na mazingira bora na rafiki ambayo alisema kwa sasa yamekosekana.
Othman ambae pia ndiye Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, alisema uwepo wa changamoto za muda mrefu katika mfumo wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika nayo ni sehemu ambayo inarudisha nyuma jitihada za kimaendeleo kwa Zanzibar.
“Sisi tunaamini mfumo wa maridhiano sawa kwa pande mbili hizi ndio suluhisho pekee kumaliza changamoto hizi,” alisema.

Pamoja na hayo Othman alisema harakati za madai haya hazikuanza leo tangu uhai wa Almarhoum Maalim Seif lakini wapo waliopinga kwa sababu za ubinafsi wao na kueleza kuwa wao hawapaswi kukaa kimya wataendeleza harakati hizo.
Akitaja sababu zilizomsukuma yeye kuchukua fomu ya Urais ni kuleta usawa kwa wananchi wote pamoja kukataa kuona wananchi wakipoteza maisha na wengine kubaki kuwa vilema hadi sasa.
“Kwa mfano hadi leo hii bado tunawakumbuka wenzetu 21 waliouwawa na vyombo vya dola katika uchaguzi mkuu uliopita,” alisema.
Aidha alisema ikiwa Zanzibar itaendelea kuongozwa kama ilivyo sasa itapoteza sifa na haiba yake na ndio maana yeye na wenzake wameamua kuinusuru Zanzibar kupitia rasilimali zake kama nchi ya visiwa.
Sambamba na hilo amesema kuna haja kubwa ya kubadilisha mifumo ya kikatiba na sheria kuondoa mamlaka makubwa aliopewa Rais wa Zanzibar na kuipa nafasi mihimili muhimu kufanya kazi zake.
Pia amesema ipo haja ya kujenga umoja wa kweli wa kitaifa utakaojenga usawa wa kidemokrasia pamoja na kupambana na ufisadi kwenye ofisi za umma.
Huku hayo yakijiri katika hatia nyingine Othman amesema iwapo watawala wataweka mazingira yasiokua rafiki watahamaisha umma kudai hai yako.
“Tunapenda watawala wajue kwamba zama za kupora wananchi hako yao zimepitwa na wakati na sasa tupo tayari,” alisema.
ZINAZOFANANA
Chadema: Tundu Lissu yupo gerezani Ukonga
Dk. Kimei aweka rekodi ya utendaji Vunjo
ACT Wazalendo yajizatiti kulinda thamani ya kura za wananchi