April 16, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Othman akabidhiwa mazito ACT Wazalendo

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman

 

MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman leo amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais wa Zanzibar huku akikabidhiwa majukumu ya msingi ya kuyatekeleza akishaapishwa. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, anakabidhiwa fomu miezi mitano tangu alipotangaza rasmi nia ya kuwania wadhifa huo mkubwa zaidi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Akiwa mbele ya vyombo vya habari ukumbi wa Hoteli yq Golden Tulip Uwanja wa Ndege hapa, Othman alisema anakusudia kushika dhamana ya kuiongoza nchi ambayo inahitaji kurudishwa mamlaka yake ikiwa njia ya kutambua utambulisho wa Wazanzibari wenye historia ndefu.

Akihutubia viongozi mbalimbali wa chama, Makamu Mwenyekiti Ismail Jussa Ladhu alisema matumaini ya watu ni kurudisha mamlaka kamili ya nchi.

Jukumu la pili ni kuunagnisha watu wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Jussa alisema Zanzibar inataka kiongozi ambaye anatambuliwa kokote aendako na kupewa hishma inayomstahili kiongozi wa dola.

Alitaja jukumu la tatu kuwa ni kuibadilisha nchi kufikia kiwango cha uchumi na maisha mazuri ya watu wake mfano wa ilikofika Singapore ilioko Kusini Mashariki mwa Asia.

Jukumu la kuigeuza nchi Singapore ya Afrika, anasema Jussa linahusisha kuwa na kutekeleza kwa ufanisi sera zitakazozalisha ajira ili kunufaisha kundi kubwa la vijana wanaoathirika kwa umaskini kutokana na ukosefu wa ajira.

Jussa anasema Rais wa Zanzibar chini ya ACT Wazalendo lazima awezeshe wananchi kuishi na furaha na raha huku wakihudumiwa kwa usawa na serikali waliyoipa mamlaka kupitia uchaguzi wa vigezo vya kuwa huru na wazi.

“Uliahidi kuwa utafika wakati utalipasua shipa. Wakati ndo huu, umma uelezwe ni vipi serikali itadhibiti ufisadi na kushughulikia mafisadi wanaokwapua mabilioni ya fedha pasina kuguswa,” alisema.

“Ukisimamia haya mara tu ukishakalia kiti cha Ikulu ya Mnazimmoja tutakuhakikishia ushirikiano kamili… utakuwa rais ambaye anaonesha khasa yale aloyapigania miaka yote Maalim Seif Shariff Hamad aliyefariki dunia akiwa hajakamilisha azma yake ya kuiongoza Zanzibar kiungwana kwa maslahi ya watu wote,” alisema.

Othman alikabidhiwa fomu kwenye Ofisi Kuu ya Chama Vuga, na Katibu wa Idara ya Uchaguzi ya chama, Muhene Said Rashid mbele ya viongozi waandamizi wa chama akiwepo pia Mke wa Othman, Mama Zainab Kombo.

Akihutubia mkutano wa viongozi kwenye ukumbi wa Majid Kiemebsamaki, Mwenyekiti Othman amesema kuchukua kwake fomu hakuna lengo la kutimiza ndoto au hamu yake kuongoza, bali ni kukubali kubeba dhamana aloachiwa baada ya Maalim Seif kutangulia mbele ya haki kabla ya kukamilisha safari aloianzisha na kuiendeleza kwa sehemu kubwa ya maisha yake.

“Tushirikiane na mimi niko tayari. Tusimamie amana na dhamana ya kukidhi matumaini ya Wazanzibari. Najua wapo wengi wanaitarajia ACT Wazalendo kukamilisha safari na Inshallah tutashinda,” alisema.

Alisema kwa wale wanachama waliochukua fomu za kuwania nafasi za majimboni na udiwani, alisema hakuna sababu ya kuvurugana kwa sababu walioasisi harakati za kuihami nchi na kuendelea kudhulumiwa kifisadi, hawakujali vyeo wala harakati zao hazikulenga kwa wao kugawana vyeo.

Waasisi wa mageuzi Zanzibar hasa wale waliofukuzwa CCM mwaka 1987, walikuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama baadhi wakiwa mawaziri na wakuu wa mikoa.

Wenzake walofukuzwa kwa tuhuma za uasi ni Ali Haji Pandu, Soud Yussuf Mgeni, Dk. Maulid Makame, Hamad Rashid Mohamed, Khatib Hassan Khatib, Shaaban Khamis Mloo, Mzee Juma Ngwali.

About The Author

error: Content is protected !!