
Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeadhimia kutoshiriki vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa kuanzia kikao cha tarehe 12 na 13 Machi, 2025 kwa sababu Baraza limepoteza uhalali baada ya kushindwa kuwa jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na Vyama vya Siasa. Anaripoti Apaikunda Mosha, Dar es Salaam … (endelea).
Kufuatia taarifa iliotolewa na katibu mkuu wa chama hicho Ado Shaibu leo 11 Machi 2025 inaeleza kuwa baraza hilo limegeuzwa kuwa jukwaa la kutumika kuhalalisha na kusafisha uchafuzi na wizi katika chaguzi kama ilivyokuwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
Aidha taarifa imeeleza kuwa kwenye kikao kilichofanyika tarehe 11 Oktoba 2024 Jijini Dodoma maazimio mbalimbali yalifikiwa kuboresha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini serikali imepuuza maazimio ya Baraza la Vyama vya Siasa ya kuboresha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
“Serikali, kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitoa ahadi ya kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa. Kinyume na ahadi yake ambayo ilitolewa kimaandishi, Serikali illyatupa mapendekezo ya Baraza la Vyama vya Siasa na kuendelea na mpango wake wa kudhulumu sauti ya wananchi kupitia wizi wa kura na uchafuzi kama ilivyoshuhudiwa nchi nzima,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha Chama hicho kimeitaka Serikali kuweka mezani kalenda ya utekelezaji wa mapendekezo ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi, pamoja na marekebisho mengine ya Sheria za Uchaguzi ikiwemo Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na pia mabadiliko madogo ya Katiba yatakayopelekea kufanyika kwa Uchaguzi Huru na wa Haki.
Pamoja na hayo taarifa inaeleza kuwa Chama cha ACT Wazalendo kimewasilisha tena kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye ndiye Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa uchambuzi wake wa kina wa masuala yanayohitaji kufanyiwa maboresho katika tasnia ya siasa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu 2025 unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
Taarifa hiyo inasema kuwa kinyume na hapo, ACT Wazalendo haitakubali kutumika kuhalalisha na kusafisha uchafu unaoandaliwa ili kupora mamlaka ya wananchi ya kuchagua na kuwaweka madarakani viongozi wanaowataka kama yalivyo matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 9 ya Katiba ya Zanzibar.
ZINAZOFANANA
TMA yatangaza uwepo wa Kimbunga ‘JUDE’ rasi ya Msumbiji
Tanzania kununua umeme Ethiopia
Kamati ya Ligi yaufuta mchezo wa Yanga na Simba