March 6, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Korea Kusini kuchangia USD Mil 104 maboresho ya Muhimbili

 

SERIKALI imedhamiria kuboresha Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuijenga upya, serikali ya Tanzania pamoja na Korea kusini kuchangia ujenzi wa mradi huo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma zote ndani ya jengo moja. Anaripoti  Mwandishi Wetu. Dodoma … (endelea).

Hayo yameelezwa leo tarehe 6 Machi 2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Rachel Mhaville kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mafanikio ya kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Amebainisha kuwa mradi huo utasongeza eneo la vitanda 1,757 kutoka 1,435 vya sasa na utagharimu USD 468 milioni (takribani Tsh. 1.2 trilioni) ambapo kati ya fedha hizo USD.364 milioni zitatoka Korea Kusini na Serikali ya Tanzania itachangia USD. 104 Milioni.

Aidha, kwa sasa upembuzi yakinifu wa mradi huo umekamilika hivyo hatua mbalimbali za kusaini mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Korea zinaendelea vizuri.

Mkurugenzi Huduma ya Upasuaji Muhimbili, Dk. Rachel Mhavile

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa awamu moja ambao utachukua miaka mitano kukamilika baada ya kusaini mkataba, hatua hii haitaathiri utoaji wa huduma hospitalini hapa hivyo huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida.

“Utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria katika sekta ya afya nchini na Ukanda wa Afrika, utakua na faida lukuki ikiwemo kuboreshwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa na kwamba Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, kuwezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa na mpangilio mpya wa hospitali huku eneo kubwa likibaki wazi kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo,” amesema Mhaville.

Aidha amesema kuwa hospitali ya Taifa Muhimbili yenye kampasi mbili ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini ina vitanda 2,043 ambapo Upanga kuna vitanda 1,435 na Mloganzila vipo 608, katika kampasi zote mbili wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku.

About The Author

error: Content is protected !!