
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jacobs Mwambegele
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jacobs Mwambegele, amesema kuwa uboreshaji wa uandikishaji wa wapiga kura mwaka huu utahusisha matumizi ya teknolojia ya Biometric Voters Registration( BVR) ambao humtambua mtu na kumtofautisha na mwingine kwa kuhusisha alama za vidole, picha na saini. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo tarehe 5 Machi 2025, jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa Tume na wadau wa uchaguzi, amesema Tume imeendelea na uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambapo uzinduzi wake ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 24 Julai 2024.
“Uzinduzi huo ulienda sambamba na uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi, hadi leo tarehe 5 Machi 2025 tume imekamilisha daftari la wapiga kura katika mikoa 28…Aidha zoezi la uboreshwaji wa daftari katika mkoa wa Morogoro na baadhi ya maeneo ya Tanga lilianza 1 Machi 2025 bado linaendelea na litakamilika tarehe 7 machi 2025”, amesema Mwambegele.
Mwambengele amesema zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkoani Dar es Salaam utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo wapiga kura wapya 643,420 wanatarajiwa kuandikishwa.
Aidha amewasa wananchi kuepuka kujiandikisha zaidi ya mara moja na kuwataka kujiandikisha kwenye kituo kimoja ili kuepuka uvunjaji wa sheria, kwani ikitokea uvunjifu wa sheria muhusika atatakiwa kulipa faini, kutumikia kifungo cha miezi sita mpaka miaka miwili au vyote kwa pamoja.
Mwambegele amesisitiza kwamba kadi ya mpiga kura iliyotolewa mwaka 2015/2020 ni halali na itaendelea kutumika katika chaguzi zijazo, hivyo zoezi la kuboresha daftari la wapiga kura halihusishi watu wenye kadi hizo au wale ambao kadi zao hazija haribika, kupotea au kuhama kutoka emeo moja kwenda lingine.
Vilevile, Tume imeweka utaratibu maalum kwa makundi maalum ya wahitaji, ambapo watapewa fursa ya kuhudumiwa bila ya kupanga foleni. Tume inaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi na wadau wote katika kuhakikisha uchaguzi unaenda vizuri na kwa haki.
ZINAZOFANANA
ACT Wazalendo kuwashitaki wateule wa Rais Mwinyi
Waziri Mkuu Majaliwa aweka jiwe la msingi bwawa la Kidunda
Puuzeni propaganda za upinzani uchaguzi utafanyika – Makalla