
Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo
KATIBU Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesema Halmashauri Kuu ya Chama hicho imeazimia kuwa kipaumbele chao cha kwanza ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini ili kuhakikisha haki inatendeka. Anaripoti Apaikunda Mosha. Dar es salaam… (endelea).
Amezungumza na leo tarehe 24 Februari 2025 na waandishi wa Habari katika Makao Makuu ya chama hicho, akieleza namna ambavyo halmashauri kuu imeweka mikakati ya kuhakikisha inapigania haki na mageuzi ya mfumo wa uchaguzi nchini ili kulinda kura ya kila mwananchi.
Amesema Halmashauri Kuu imetaka wadau wake kuendeleza ushirikiano na vyama vingine makini vya upinzani na wadau wengine wa demokrasia zikiwemo asasi za kiraia na viongozi wa dini katika kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi hapa nchini.
Amesema ACT walimpa Rais Samia ushirikiano katika kuleta mageuzi lakini bado hayakutekelezwa hivyo wamejiridhisha kwamba maridhiano yaliyoaahidiwa yamesambaratika na falsafa yake ya 4R imeota mbawa, basi wanamtaka rais kufanya tathmini juu ya ahadi anazozitoa kwa maneno na kukosekana kwa utekelezaji wake.
Ado amesema Rais ajiulize swali muhimu, yanapojengwa mazingira ya kutoaminika kwa ahadi zake watanzania wamwamini nani? Ameendelea kusisitiza kuwa kwa tathimini ya chama cha ACT Wazalendo, katika 4R zote alizoahidi Rais tunaona hakuna utashi wa kisiasa wa kutekeleza ahadi hizo kwa vitendo.
“Katika uchaguzi wa serikali za mitaa chama chetu kimekusanya visa na matukio mengi ya uvunjifu wa haki za binadamu, watu wetu wamegombea na wanachama wetu zaidi ya 300 wamekutana na visa vingi,” amesema Ado.
Amesema kwa upande wa Zanzibar, ACT wana ripoti ya mauaji 21 yaliyofanyika wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, na baada ya uchaguzi walitoa muhtasari wake, hata hivyo wanawafahamu waliouwawa na baadhi ya watu ambao walishiriki na kuratibu kwenye mambo hayo.
Aidha, Halmashauri Kuu imelekeza chama kifanye uchambuzi na kutoa ripoti ya kina juu ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu nchini vilivyofanywa na vinavyoendelea kufanywa na ripoti hizo zipelekwe kwa wadau wa demokrasia wa ndani na kimataifa ili waweke mkakati wa pamoja wa kupeleka mashtaka kwenye mahakama za kimataifa ili haki itekelezwe.
Pamoja na hayo amesema kuwa Halmashauri Kuu imeelekeza chama kuandaa operasheni ya kulinda demokrasia nchini itakayojulikana kama ‘Oparesheni Linda Demokrasia’ ili kuhamasisha umma kupigania haki zao na kutokubali kuwa wanyonge ili uchaguzi uwe huru wa haki na kuaminika.
ZINAZOFANANA
Makamba amhakikishia Rais Samia kushinda kwa kishindo Lushoto
Samia azindua jengo jipya la Halmashauri ya Bumbuli
Samia: Uhitaji wa kahawa duniani ni fursa kwa Afrika