![](https://mwanahalisionline.com/wp-content/uploads/2025/02/473591306_2031074124058510_948167479327298360_n.jpg)
Kanali Gaudentius Gervas Ilona
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa taarifa kuwa wanatarajia kushiriki mazoezi mbalimbali ya kijeshi ya pamoja baina ya nchi rafiki Duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Haya yameelezwa kwenye taarifa iliyotolewa leo tarehe 7 Februari 2025 na Kanali Gaudentius Gervas Ilona, kaimu mkurugenzi wa habari na uhusiano jeshi la ulinzi la wananchi Tanzania.
Ameeleza kuwa katika ushiriki wa “JWTZ kwa sasa linaendelea na maandalizi ya mazoezi mawili ya kijeshi yatakayofanyika hapa nchini yanayojulikana kama ‘ Justified accord’ na ‘Cutlass Express’ yatakayoshirikisha Jeshi la Marekani na majeshi mengine ya nchi kumi na mbili (12)”
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, “zoezi la kijeshi ‘Justified accord’ ni zoezi la nchi kavu linalotarajiwa kufanyika eneo la Chalinze Mkoa wa Pwani na Nananyuki nchini Kenya kuanzia tarehe 10 Februari 2025 kwa ushirikiano kati ya Tanzania na nchi ya Marekani.”
Pia, “zoezi hili litazinduliwa rasmi tarehe 10 Februari 2025 na linatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 21 Februari 2025. Kufanyika kwa zoezi hili kutatoa fursa kwa vikundu shiriki kuongeza weledi na uelewa wa pamoja wa kupambama na matishio mbalimbali ya kiusalama kama vile matishio ya kiugaidi”.
“Zoezi hili lingine la ‘Cutlass Express’ ni zoezi ambalo litafanyika kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja na ushirikiano katika kukabiliana na matishio ya Ulinzi na Usalama katika maeneo yetu ya uwajibikaji baharini ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa Madawa ya Kulevya.”
Aidha ameeleza kuwa “zoezi hilo ni la wanamaji linatarajiwa kufanyika katika nchi za Tanzania, Madagascar na Ushelisheli kuanzia tarehe 10 Februari 2025 na kufungwa tarehe 21 Februari 2025 ambapo kwa Tanzania litafanyika katika jiji la Tanga na litashirikisha nchi kumi na nne (14) ikiwemo Marekani ambayo inashirikiana na Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania katika maandalizi ya mazoezi hayo hapa nchini”.
“Nchi waalikwa katika zoezi hilo ni pamoja na Kenya, Madagascar, Shelisheli, Djibuti, Comoro, Georgia, Msumbiji, Malawi, Mauritius, Tunisia, Somali na Senegal”.
Aidha amewaarifu wananchi kuwa watulivu kwani “katika Mazoezi hayo wanatarajiwa kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya Ndege Vita na Meli Vita, hivyo wananchi wanataarifiwa kutokuwa na taharuki.”
ZINAZOFANANA
Dk. Abbas ahimiza malikale kidijitali
Tanzania yapewa uenyeji mkutano wa kikanda Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Afrika
Siku nane kumaliza tatizo la maji Tabata, Ukonga, Kinyerezi