NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula ana wakati mgumu kutetea jimbo lake la Mkinga, Tanga kwa kinachoelezwa ni kukwama utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyoahidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tanga … (endelea).
Hali hiyo ilibainishwa mwishoni mwa wiki na baadhi ya wananchi waliosema hawaridhishwi na mwenendo wa mbunge huyo, aliyeshikilia jimbo hilo kwa miaka 15 sasa.
Kitandula alipotafutwa kujibu madai hayo, hakupatikana, lakini Katibu wake, Mohamed Nondo alisema anahitaji muda kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, baadaye alipotumiwa ujumbe wa maneno kuhusu malalamiko ya wananchi wake, Kitandula alitaka aorodheshewe malalamiko hayo, ili ayajibu, alifanyiwa hivyo na Gazeti lakini mpaka tunakwenda mitamboni hakuwa amejibu.
Uchunguzi wa Gazeti hili, umebaini kuwa moja ya malalamiko ya wananchi wa jimbo hilo ni ubovu wa barabara ya Tanga-Maramba-Daluni hadi Mashewa ya kilometa 78.
Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii, analalamikiwa kutofanya ziara za kata, vijijini na vitongojini kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha, ili ajionee na kufanya tathimini ya viwango vya utekelezaji vilivyofikiwa.
“Kwa miaka 15 tumempigia kelele mbunge na aliahidi kumaliza kero hiyo kila alipokuja kuomba kura, safari hii sijui atakuja na lugha gani ili tumwelewe,” alisema mkazi wa kijiji cha Pangalawe.
Mwanakijiji huyo aliendelea kumlaumu Mbunge kuwa hatembelei wananchi wa eneo lake la kiutawala kusikiliza kero zao, ili kushiriki kutafutia ufumbuzi wa kudumu.
“Hafanyi mikutano ya hadhara, hiki ni kitu ambacho kwa miaka yote 14 ya utawala wake hakijawahi kutokea hata kwa nadra, kitu ambacho kimefanya Mkinga kama jimbo, kukosa vipaumbele vya pamoja ambavyo vingechochea mabadiliko ya wananchi,” alilalamika.
Kitandula aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, mara ya kwanza aliingia bungeni mwaka 2010, akipokea kijiti kutoka kwa Mbarouk Mwandoro.
Kabla ya Mwandoro, jimbo hilo liliongozwa na Luka Kitandula ambaye ni baba mzazi wa Danstan.
“Kwa hiyo kwa miaka 15 aliyokaa, Danstan ameshindwa kutimiza ahadi ya ujenzi wa barabara hiyo nyeti kwa matumizi wa wananchi, sina hakika kama atagombea tena, lakini kwa hali ilivyo, bora asigombee au sisi tufanye mabadiliko, miaka 15 inamtosha,” alisema Khadija Mussa.
Akiwa na wanawake wengine wakihaha kupata maji katika kijiji cha Jirihini, alitaja kero nyingine kuwa ni shida kubwa ya maji lakini pia huduma za afya.
Alisema maji wanayopata, yamechimbwa na kampuni binafsi iliyojenga visima vya umeme zaidi ya 20 katika baadhi ya maeneo ya jimbo.
Mmoja wa viongozi wa CCM wa kijiji cha Gombero, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema tatizo la Mbunge wao ni kutoonekana wala kufanya vikao na wananchi.
Baadhi ya wananchi wanaamini kuwa kutofanya ziara kwa Mbunge huyo jimboni, kumesababisha baadhi ya miradi kutokamilika kwa wakati na kwa kiwango tarajiwa.
Mradi wa maji wa Bwiti-Mavovo uchimbaji mtaro, uunganishaji mabomba havijafanyika lakini mkandarasi Local Fundi, amelipwa na hayupo eneo la kazi kwa zaidi ya miezi sita sasa.
Mwingine ni Dalumi Kisiwani A na B uliotekelezwa kupitia mkandarasi, lakini miundombinu ya kuingiza maji kwenye tangi ina udhaifu.
“Kuna vifaa vilivyopaswa kuwekwa havijawekwa, mipira iliyopaswa kuunganishwa na kufukiwa kama ilivyotakiwa haijakamilika, mradi unasuasua. Mkandarasi amelipwa na hayupo eneo la kazi wananchi kuteseka,” alibainisha kiongozi huyo wa CCM.
Mradi wa tatu ni Maramba ambako Serikali iliingiza fedha za ukarabati, lakini haujakamilika, kwani ulitakiwa kwisha na kukabidhiwa Septemba mwaka jana.
Upo mwingine wa maji wa Kigongoi-Vuga ambao nao uliingiziwa fedha za ujenzi wa tangi, vituo vya kuchotea maji na ulazaji mabomba.
“Cha ajabu mkandarasi aliyekabidhiwa miradi ambayo hajakamilisha, amepewa pia mradi huu, una zaidi ya mwaka hautoi maji, amelaza mabomba hayajaungwa mengine yamejaa uchafu. Wananchi wanahangaika na hakuna majibu sahihi juu ya hatima ya mradi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mradi mwingine ni Mhinduro uliokabidhiwa kwa mkandarasi, ujenzi wa tangi ulishaanza kwenye chanzo cha maji, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea.
Miradi mingine ni Gombero na Mapatano, ambayo imekwama kutokana na changamoto za kiuongozi hasa usimamizi wa karibu.
ZINAZOFANANA
‘Honey Moon’ yenu ikija na mambo ya hovyo hatukubali – Wassira
Tuwakatae wanasiasa wachonganishi na wafitinishi – Makalla
Tanzania yaweka mkazo mkakati wa nishati ya kupikia