RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati bora na safi ya kupikia, hatua ambayo itaboresha afya, kulinda mazingira, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kusambaza nishati ya umeme, huku juhudi sasa zikihamia kwenye utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
“Mpango wetu wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unalenga kuondoa utegemezi wa nishati isiyo safi na yenye madhara kwa afya. Lengo ni kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2030,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alieleza kuwa Tanzania imefanikiwa kupeleka umeme katika vijiji vyote 12,318 na vitongoji 32,827. Kazi ya kufikisha umeme kwenye vitongoji vilivyobakia 31,532 inaendelea kwa kasi, huku serikali ikiongeza uzalishaji na kuboresha miundombinu ya usambazaji wa umeme.
“Tunapoongeza upatikanaji wa umeme, pia tunazingatia matumizi ya teknolojia za kisasa zinazosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, ambazo zimekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira na hatari kwa afya ya wanawake na watoto,” aliongeza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alitaja juhudi za Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa nishati kwa nchi jirani kama Burundi, Rwanda, na Kenya, huku juhudi za kuunganisha umeme na Zambia pamoja na Uganda zikiwa katika hatua za mwisho.
Awali, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alipomkaribisha Rais Samia kuhutubia, alieleza kuwa juhudi za serikali zimeongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,888 hadi 3,431, hatua ambayo imeimarisha nafasi ya Tanzania katika kuendesha ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Mkutano huu wa kihistoria, unaohusisha viongozi wa Afrika na wadau wa maendeleo, unahitimishwa leo Januari 28, 2025, ukijadili mikakati ya pamoja ya kuhakikisha wananchi wa Afrika wanapata nishati salama na endelevu.
ZINAZOFANANA
‘Honey Moon’ yenu ikija na mambo ya hovyo hatukubali – Wassira
Dk. Biteko aongoza waombolezaji kuaga miili ya wanafunzi waliokufa kwa radi
Wanawake vyombo vya ulinzi na usalama Songwe kushiriki Siku ya Wanawake Duniani