January 18, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk Slaa azidi kusota jela, wakili wake ageuka mbogo

Dk. Wilbroad Slaa

 

WAKILI Peter Madeleka, ambaye ni mmoja wa mawakili sita wanaomtetea aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Sweeden Dk. Wilbord Slaa amelaumu utaratibu wa uendeshaji kesi ya mteja wake hivyo kubisha hodi Mahakama Kuu kuomba mapitio ya shauri hilo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Madeleka amesema haridhishwi na mteja wake kunyimwa dhamana ambayo ni haki yake.

Wakili Madeleka amesema hayo, leo tarehe 17 Januari, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya ombi la kuzuia dhamana ya Dk. Slaa kutosikilizwa mahakamani hapo.

Wakili Madeleka amesema kuwa walikuwa wana muda wa kutosha kusikiliza na kuamua dhamana ya Dk. Slaa lakini hakimu anayeshikilia shauri hilo akaamua kuahirisha mpaka tarehe 23 Januari, mwaka huu ambapo atatoa uamuzi wa mapingamizi kwenye shauri la msingi.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki baada ya kusikiliza ombi la upande wa utetezi la kuitaka mahakama iifute kesi Na.993 ya mwaka 2025 inayomkabili Dk. Slaa yenye shtaka moja la kuchapisha taarifa za uongozi kwenye mtandao wa X. Upande wa Jamhuri ulitaka mwongozo wa mahakama kama itakwenda kusikiliza pingamizi lao la dhamana ya Dk. Slaa na kuieleza mahakama hiyo kuwa maombi ya mawakili wa utetezi yanadai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa, ameiambia mahakama hiyo kuwa itoe mwongozo juu ya maombi ya kupinga dhamana ya Dk. Slaa kwa kile alichodai mahakamani hapo kuwa upande wa utetezi ulishadai mara nyingi kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hivyo ni vema wakasubiri uamuzi wa pingamizi katika shauri la msingi.

Wakati huo huo, wakili wa Utetezi Peter Madeleka aliinuka na kudai kuwa ibara ya 159B (4)b kwamba katika Mamlaka aliyokuwa nayo Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru hataingiliwa na mtu yoyote au mamlaka yoyote atazingatia kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki.

Madeleka amedai mahakamani hapo kuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa na kwamba shtaka analoshtakiwa nalo linadhaminika.

Wakati huo huo wakili Tawabu, alisimama na kudai mahakamani hapo akikazia hoja yake .

Wakili wa utetezi Hekima Mwasipu kudai kuwa Dk. Slaa ni mtu mzima umri miaka 73 hawezi kuhimili vishindo vya mahabusu halkadhalika ni mgonjwa .

Hoja hiyo ikamnyanyua Rais wa Wanasheria Tanganyika (TLS ), Boniface Mwabukusi ambaye alikuwa akiongoza jopo la mawakili utetezi alidai kuwa wajibu wa mahakama ni kuhakikisha haki inatendeka huku akibainisha kuwa Dk. Slaa ni mtu mzima anayeumwa na ana haki ya dhamani “hii sasa wiki moja anasota mahabusu, nyie mawakili wa serikali ni vijana lakini siku mbili tu mahabusu hamtaweza kwanini asipewe haki yake ya kupata dhamana ”

Baada ya ubishani wa kisheria, sauti ya ahirisho la mahakama ilisikika kutoka kwenye kinywa cha Polisi na kuashiria kuahirishwa kwa shauri hilo hadi tarehe 23 Januari 2025 ambapo utatolewa uamuzi wa mashauri ya maombi yote lile la kuzuia dhamana na lile la kutaka kesi ifutwe kwa kuwa haina uhalali .

Dk. Slaa ataendelea kuwa mahabusu mpaka pale ombi lake la dhamana litakaokubaliwa ambapo Hakimu Beda amesema tarehe 23 Januari atatoa uamuzi.

About The Author

error: Content is protected !!