MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Sebastian Waryuba, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Khamis Katimba kwa kukusanya asilimia 82 ya mapato ya ndani katika miezi sita pekee (Julai – Desemba 2024). Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo tarehe 4 Januari 2025, Waryuba ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema pamoja na kiwango hicho kizuri cha makusanyo, lazima ijulikane zinatumikaje.
“Nimefurahi kushuhudia kasi hii ya ukusanyaji mapato bila kutoana damu, mabadiliko haya yanaonesha safari ya huku tuendako tutaifika salama. Lazima fedha zionekane zimefanya nini, hili ni jambo la msingi kabisa,” alisema.
Akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo ya Waryuba, Mkurugenzi Katimba alisema wananchi wakiona fedha zao zinafanya kazi gani, watahamasishana.
“Mimi nawaahidi, wao kazi yao ni kulipa kodi halafu waje waniwajibishe kwa matumizi ya fedha zao. Nawaomba waendelee kulipa kodi ya serikali lakini waje kuniwajibisha kwa matumizi ya fedha zao.
“Ofisi yangu ipo wazi kwa wote, hata akija mmoja mmoja naruhusu aje ofisini kwangu, aje aniulize umekusanya shilingi ngapi na umetumia shilingi ngapi, nitamueleza. Ofisi ipo wazi, ni ofisi ya wananchi wote, sisi ni dhamana tu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Pius Mwelase alisema, katika uhai wa halmashauri hiyo, haijawahi kutokea kukusanya mapato ya ndani asilimia 82 katika kipindi cha miezi sita pekee.
“Haijawahi kutokea mpaka Desemba kukusanya 82% kwenye halmashauri yetu, viporo vyote toka halmashauri yetu ianze tunavimaliza na kama kuna vingine semeni, sasa pesa ipo.
“Ubunifu aliokuja nao mkurugenzi wetu umeleta mabadiliko makubwa mno, tunajivunia na tunaamini bado tuna muda wa kutosha wa kukusanya fedha zingine nyingi kutokana na mikakati iliyopo kwa sasa,” alisema.
ZINAZOFANANA
Makala apata kigugumizi kinachoendelea Chadema
CCM yampongeza Mkurugenzi wa shule za Tusiime
Ushindi wa Profesa Lipumba wapingwa