December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba, 2024 liliwashikilia watuhumiwa 2,827 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka 2023 ambapo jumla ya watuhumiwa 3,238 walikamatwa ikiwa ni pungufu ya watuhumiwa 411 sawa na 6.8% kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya Ukatili wa kijinsia, Uvunjaji, Wizi, mauaji, utapeli kwa njia ya mtandao, dawa za kulevya, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali za vifo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Songwe … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na SACP Augustino Ignace Senga, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Songwe, imeeleza katika kipindi hicho limeendelea kupata mafanikio mahakamani kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali kuhukumiwa ambapo jumla ya watuhumiwa 327 wamepatikana na hatia, 37 wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 jela kwa kosa la kubaka na watuhumiwa 14 wamehukumiwa vifungo vya Maisha jela kwa kosa la kulawiti na kubaka, watuhumiwa 17 wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 jela kwa kosa la unyang`anyi kwa kutumia silaha.

Watuhumiwa wengine 12 wamehukumiwa vifungo vya miaka 20 jela kwa kosa ya kupatikana na silaha ikiwa na risasi pamoja na nyara za serikali na watuhumiwa 227 wamehukumiwa kifungo cha mwaka 1 mpaka miaka 15 jela kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya usalama barabarani. Ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023 ambapo jumla ya watuhumiwa 238 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali sawa na ongezeko la watuhumiwa 89.

Katika muendelezo wa misako dhidi ya dawa za kulevya na pombe ya moshi jumla ya watuhumiwa 129 walikamatwa wakiwa na lita 483 za Pombe ya Moshi (gongo) watuhumiwa 100 wamehukumiwa vifungo vya miaka 3 mpaka 5 jela na kesi 29 zinaendelea mahakamani katika Wilaya ya Momba, Ileje, Songwe na Mbozi. Ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023 ambapo jumla ya watuhumiwa 87 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali sawa na ongezeko la watuhumiwa 42.

Katika kipindi hicho hicho, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe liliwashikilia watuhumiwa 43 kwa makosa ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi kilo 252 na gram 475 katika wilaya ya Momba, Ileje, Songwe na Mbozi na watuhumiwa 180 wamehukumiwa vifungo vya miaka 3 mpaka 5 jela na kesi 72 zinaendelea mahakamani pia watuhumiwa 194 wamekamatwa kwa makosa ya uvunjaji, watuhumiwa 120 wamehukumiwa vifungo vya miaka 15 mpaka 20 jela na kesi 74 zinaendelea mahakamani. Ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023 ambapo jumla ya watuhumiwa 29 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali sawa na ongezeko la watuhumiwa 14.

Katika kuelekea sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka 2025, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe tumejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao na kuendelea kuimarisha Misako na Doria za Magari, Miguu na Mbwa wa Polisi katika maeneo yote hususani kwenye makazi ya viongozi, makazi ya watu, nyumba za ibada (Misikiti na Makanisa], Barabara kuu, kumbi za starehe na maeneo yote tete. Vile vile tumejipanga vizuri kuendelea kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa makundi mbalimbali ya jamii, madereva wa vyombo vya moto, wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, Wanavyuo na wananchi kwa ujumla.

Pia kuwajengea uwezo wa kujilinda na kuchukua tahadhari wawapo katika maeneo mbalimbali na pindi waonapo viashiria vya uhalifu kuwa wepesi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi. Ni marufuku kwa mtu yeyote kupiga/kulipua milipuko (Fataki) bila kuwa na kibali cha Jeshi la Polisi, Hadi sasa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe halijapokea ombi la mtu kutaka kupiga fataki katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, hivyo hatutegemei kuona wala kusikia mtu anapiga fataki.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kujali suala la ulinzi na usalama wa mtoto [Sheria ya mtoto 2009] inaeleza wajibu wa mzazi kwa mtoto ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi, kumuepusha na vihatarishi na mazingira hatarishi kwake. Hatutegemei kuona Watoto wanazurura hovyo mitaani bila kuwa na uangalizi, kwenye sehemu za michezo ya watoto tunatarajia kuwaona wazazi/walezi wakiwa na Watoto wao ili kuangalia usalama wao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe litaendelea kufanya doria maeneo yote ya kumbi za starehe na kwenye mikusanyiko ya michezo ya Watoto kwa kuimarisha ulinzi lakini tunawataka wamiliki wa maeneo hayo kuweka walinzi na waangalizi kwani katika kipindi hiki tunategemea watu wa rika tofauti Kwenda katika maeneo hayo na Wamiliki wa kumbi hizo kuhakikisha kuimalisha ulinzi hususani kwenye maegesho ya magari. Kuhakikisha wanajua uwezo wa kumbi zao ili kuepuka kuzidisha watu na kusababisha madhara ya kibinadamu.

Kipindi hiki tutakuwa wakali sana, tumeshatoa elimu kwa kiwango kikubwa na tunaendelea kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara. Tunategemea utii wa sheria za usalama barabarani bila shuruti, madereva kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe ni marufuku kwa Dereva kutumia kilevi, tutakuwa na kipima ulevi katika maeneo mbalimbali, atakayebainika kuendesha chombo cha moto akiwa ametumia kilevi, pia atakaye bainika kutokuwa na leseni hai ya udereva hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linazidi kusisistiza na kutoa wito kwa wazazi/walezi kutimiza wajibu wao kwa kuweka uangalizi makini kwa Watoto, kushindwa kutimiza wajibu wao na kupelekea madhara kwa Watoto sisi Jeshi la Polisi hatutakaa kimya, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika.

Aidha, tunaendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na kuwataka kutambua kuwa jukumu la ulinzi ni letu sote hivyo tushirikiane kubaini, kuzuia na kutokomeza uhalifu. Vilevile, katika maeneo ya nyumba za ibada tunaendelea kusisitiza suala la ulinzi binafsi na kupanga watu maeneo ya nje kwa ajili ya kuangalia usalama wa vyombo vya moto Magari na Pikipiki bila kusahau ulinzi jirani ili kuweza kusherehekea sikukuu vizuri na kuukaribisha mwaka mpya bila ukatili wala uhalifu katika Mkoa wetu.

Mwisho, niwatakie wananchi wote wa Mkoa wa Songwe maandalizi mema ya Sikukuu ya Kristmas na Mwaka mpya 2025.

About The Author

error: Content is protected !!