December 12, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tuendelee kutumia teknolojia katika uhifadhi – Dk. Abbasi

 

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi ameelekeza kuendelea kwa matumizi ya teknolojia mbalimbali katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Dk. Abbasi ameyasema hayo leo tarehe 10 Desemba, 2024, katika kikao na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kilichofanyika katika Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro.

“Tuendelee kutumia teknolojia za kisasa katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori,” amesema Dk. Abbasi.

Aidha, Dk. Abbasi ameipongeza TAWA kwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma mnamo mwezi Septemba ya kununua ndege nyuki kwa ajili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi

“Nimefurahi kuona mmeanza kutekeleza maelekezo ya Rais ya kununua ndege nyuki na hapa TAWA nimeona kazi imeanza,” ameongeza Dk. Abbasi

Vilevile, Dk. Abbasi alitoa pongezi kwa TAWA kwa ujenzi wa vizimba sambamba na ujenzi wa mabwawa katika Hifadhi ya Rungwa na Makuyuni ambao utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wanyamapori.

Kwa upande wake, akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange alimshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwa asilimia mia moja.

“Sisi kama TAWA ni jadi yetu kutekeleza maelekezo bila kupindisha,” amesema Kamishna Kabange.

Kuhusu matumizi ya teknolojia, Kamishna Kabange ameongeza kuwa TAWA imenunua ndege nyuki 11 kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na itaongeza nyingine zaidi, sambamba na kutafuta teknolojia zingine zitakazosaidia katika shughuli za uhifadhi.

Awali, Dk. Abbasi alipata wasaa wa kuangalia onesho la matumizi ya ndege nyuki katika kumrudisha tembo hifadhini sambamba na kukabidhiwa kombe la SHIMMUTA kwa upande wa mashindano ya Kamba na Riadha.

About The Author

error: Content is protected !!