KATIBU wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki amekutwa amefariki kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kuhudhuria semina elekezi kwa Makatibu jijini Dodoma kesho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Amos Makalla leo tarehe 13 Novemba 2024, chama hiko kimeoneshwa kusikitishwa na tukio hilo, sambamba na kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu, viongozi na wanachama wa chama hiko.
“Chama Cha Mapinduzi kinatoa pole kwa familia, ndugu, viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa kufuatia kifo cha ghafla na cha kikatili.” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha katika taarifa pia Chama hiko, kimewataka wanachama wake kutulia, wakati muda huu vyombo vya usalama vikichunguza tukio hilo, ili wahusika waweze kufikishwa katika vyombo vya kisheria.
“Tunawaomba wanachama wetu wawe watulivu wakati vyombo vya dola vikifuatilia na kuchunguza tukio hili, ili wahusika waweze kufikishwa katika vyombo vya kisheria.”
Taarifa ya kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa SACP Allan Bukumbi, imesema kuwa tayari jeshi hilo limeshaanza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, lililotokea tarehe 12 Novemba 2024, na kutoa rai kwa mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu waharifu hao, kuzifikisha kwenye mamlaka husika ili ziweze kufanyiwa kazi kwa watuhumiwa hao kudakwa.
ZINAZOFANANA
Morocco kuwapa wanawake haki zaidi
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani