September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Spika Tulia amfunda Kombo jinsi ya kumsaidia Samia

SPIKA wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson amemtaka Mbunge mteule, Balozi Mahmoud Thabit Kombo kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wanaendeleza mahusiano kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kimataifa.

Amesema Rais Samia anatekeleza mipango mingi hivyo, wana jukumu la kumsaidia katika kutekeleza mipango hiyo kama alivyowaamini.

Dk. Tulia aliyasema hayo leo Alhamisi katika Ofisi ndogo za Bunge zilizopo Dar es Salaam baada ya kumwapisha Balozi Kombo kuwa Mbunge ambaye aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki tarehe 21 Julai mwaka huu.

Spika alimpongeza Balozi Kombo kwa kuaminiwa na Rais katika nafasi hiyo ya ubunge kwamba nafasi hizo ni chache na kuwepo miongoni mwao ni heshima kubwa.

Alimtaka Mbunge huyo kufanya kazi kwa ushirikiano kuhakikisha taifa linasonga mbele na kufanyia kazi mipango ya Rais na kwamba wanatarajia wao wataendeleza mipango hiyo ya mahusiano ya Afrika Mashariki na kimataifa.

“Tunaamini mtaendelea kushirikiana kuhakikisha gurudumu la maendeleo ya nchi hii linaendelea kusonga mbele,” alisisitiza Dk Tulia.

Alisema kuwa Balozi Kombo ameapa kiapo cha uaminifu ambacho kinamfanya kuwa Mbunge kwa matakwa ya Ibara ya 68 ya Katiba na Kanuni ya 30 fasili ya kwanza ambayo inaeleza kabla ya mbunge kushiriki shughuli za bunge, lazima awe amekula kiapo cha uaminifu mbele ya Spika.

Pia alieleza sababu ya kumwapishia Dar es Salaam kwamba fasili ndogo ya (2) (b) ya kanuni za bunge ambazo zimefanyiwa marekwbisho, inaeleza kuwa Mbunge ataapishwa na Spika kiapo cha uaminifu eneo litakalopangwa na Spika.

“Kanuni zinaruhusu mbunge kuapishwa popote pale ambapo Spika ameagiza ikiwa ni nje ya bunge au bungeni. Leo tumefanyia Dar es Salaam lakini tungeweza kufanya sehemu nyingine yoyote na kanuni zetu zinaruhusu,” alisisitiza.

Baadhi ya wabunge walioshiriki katika hafla hiyo ni Dk. Stegomena Tax – Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dennis Londo ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Mteule.

About The Author