WAZIRI wa Maji Juma Aweso amewahakikishia wakazi wa Dar es Salaam na Pwani upatikanaji wa maji safi na salama katika mikoa hiyo kwani Changamoto ya hitilafu ya mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu juu tayari imerekebishwa.
Waziri Aweso ameyasema haya leo tarehe 28 Oktoba 2024 katika ziara ya kukagua na kutembelea mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu na kujione mwenyewe ukarabati uliofanywa na wahandishi wa Dawasa baada ya kutokea kwa hitilafu katika moja ya mitambo kiasi cha kuathiri uzalishaji wa maji safi na salama.
Amesema kwa kawaida mtambo wa Ruvu juu ukiwa katika hali ya ubora wake unazalisha maji kiasi cha lita 197milioni kwa siku , lakini baada ya kutokea kwa hitilafu uzalishaji wa maji ulikuwa katika kiwango cha chini kiasi cha lita 170milioni hivyo kuathiri upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
“Nilikuwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu nikapata taarifa za kelele za malalamiko kuhusu kukosekana kwa maji hasa katika maeneo ya malamba mawili, Saranga, Mbezi Msakuzi, Bonyokwa na maeneo mengine nikalazimika kumaliza ziara ili nije nijue tatizo ni nini” amesema Aweso.
Waziri Awezo amesema anawashukuru mafundi kutoka Dawasa kwani walihakikisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana kumaliza tatizo hilo ili wananchi waendelee kuifurahia huduma ya maji jambo ambalo tayari limeshapatiwa ufumbuzi.
“Niwahakikishie ndugu zangu wananchi, upatikanaji wa maji kwa sasa umerudi katika hali yake, mafundi wetu wameshafanya kazi usiku na mchana kumaliza tatizo hilo.”amesema Waziri Aweso.
Aidha ametoa agizo kwa wafanyakazi wa Dawasa pamoja na Wizara yake kuhakikisha kuwa hawazizoei shida za wananchi bali wahakikishe kuwa wanawapatia maji safi na salama kwa wakati kwani wakazi wa Pwani na Dar es Salaam hawana mbadala mwingine wa maji.
“Menejimenti msikae ofisini, maji hayana mbadala hivyo Dawasa timizeni wajibu wenu, hatuna kisingizio kwamba maji katika mto yapo kidogo, maji yapo ya kutosha, tuwaombe wananchi radhi kwa hii hitilafu, piteni maeneo yote tusilete visingizio:” Amesema Waziri Aweso.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon pamoja na kumshukuru waziri Aweso kutembelea katika mtambo huo amesema kwa sasa wamewekeza zaidi katika kuhakikisha kuwa mifugo haiathiri vyanzo vya maji na maji yanaendelea kutiririka kama kawaida.
Amesema siku za karibuni wameondoa zaidi ya ng’ombe 3000 katika mto Ruvu lengo likiwa ni kukilinda chanzo hicho cha maji ili maji yaendelee kutiririka na wananchi waweze kupata maji safi na salama.
“Tumeimarisha ulinzi kwenye mto wetu wa Ruvu, juzi tuliondoa zaidi ya mifugo 3000 na tayari tumeshaandaa vyanzo vingine vya kunywesha maji mifugo yetu, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam na Pwani wanaendelea kupata maji safi na Salama.” amesema DC Nickson.
Mkuu wa Wilaya Nickson amesema chanzo mama cha upatikanaji wa maji kitaendelea kulindwa kwa wivu mkubwa hasa katika kipindi hiki cha ukame, mvua zikisubiriwa tena kujaza mito na vyanzo vingine vya maji.
Hata hivyo Katibu wa siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani David Mramba amesema wiki mbili zilizopita Wizara ya maji ilituma wataalamu wake baada ya kutokea kwa hitilafu katika mtambo wa Ruvu Juu.
Amesema wataalamu hao na mafundi walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanamaliza tatizo hilo ili wananchi wa Pwani na Dar es Salaam wanaendelea kufurahia huduma ya maji safi na salama.
ZINAZOFANANA
Wafugaji watamba kuwaweka viongozi wa wilaya mfukoni
Mateso ya wazabuni Liwale, 15 wadhulumiwa malipo fedha zao
Necta watangaza matokeo ya darasa la saba 2024