November 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Kuna sababu nyingi Tamisemi kutosimamia uchaguzi

 

SISI raia watatu – Bob Wangwe, Bubelwa Kaiza na Ananilea Nkya, katika shauri tulilofungua Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kwa niaba ya Raia wa Tanzania na tayari limeshasikilizwa na hukumu ni tarehe 25 Oktoba 2024, katika kuonyesha TAMISEMI haina mamlaka kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, mawakili wetu walizingatia Sheria za nchi na msingi wa haki za asili. Anaripoti Ananilea Nkya, Dar es Salaam … (endelea).

Moja, Sheria Na. 2 ya mwaka 2024, inayoitwa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), iliyotungwa na Bunge mwaka 2024, katika kifungu cha 10(1)c kimeipa INEC mamlaka ya kuendesha, kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kazi hiyo haijapewa TAMISEMI.

Mbili, kifungu hicho cha sheria, kimeweka bayana kuwa Bunge litatunga sheria itakayotoa utaratibu wa INEC kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini haikusema ikiwa Bunge halijatunga sheria hiyo (ambapo sisi raia hatuamini ilikuwa ni kwa bahati mbaya haikutungwa), TAMISEMI itasimiamia uchaguzi huo.

Kama hiyo haitoshi, kifungu hicho au sehemu yoyote ya sheria hiyo,haikuhamisha mamlaka hayo iliyotoa kwa INEC kwamba yatatekelezwa na TAMISEMI katika mazingira yoyote.

Sheria hiyo, haikukaimisha shughuli ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa chombo kingine, ilimaanisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia mwaka 2024 utasimamiwa na INEC katika mazingira yoyote.

Hivyo ni sahihi kusema, kitendo cha Waziri wa TAMISEMI kutunga kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024), ili TAMISEMI kusimamia, kuratibu na kuendesha uchaguzi huo, sio tu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, bali ni upokaji wa mamlaka ya Bunge na INEC,tena katika mazingira ambayo waziri ameapa kulinda na kuheshimu sheria za nchi.

Tatu, mawakili wa Serikali walidai mahakamani kwamba Sheria za Serikali za Mitaa, Sura 287 na 288, zinampa Waziri wa TAMISEMI mamlaka ya kutunga Kanuni za uchaguzi.

Mawakili wa raia walijibu hoja hiyo kwamba kimsingi Waziri wa TAMISEMI alipaswa kutambua kwamba sheria mpya inapotungwa kuhusu jambo fulani, kama kulikuwa na sheria ya zamani iliyosimamia jambo hilo, kisheria ni kwamba sheria mpya inakuwa imeifuta sheria ya zamani (implied repeal) na hiyo sheria mpya ndiyo inatumika.

Mawakili wa raia wameiambia Mahakama kwamba haipaswi kukaa kimya kwenye suala la TAMISEMI kupoka mamlaka ya INEC, kwa kuwa sababu ya kuwepo kwa dhana ya implied repeal ni kusoma sheria kama inavyojieleza.

Lakini pale ambapo ukisoma sheria haileti maana au sheria moja inakinzana na nyingine, basi ni jukumu la Mahakama kutasfiri sheria kwa kuzingatia vigezo ikiwa ni pamoja na kwamba mtunzi wa sheria alikuwa na lengo gani. Hii imewahi kufanyika katika kesi ya Joseph Warioba na Steven Wasira na kesi ya BAWATA na mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Nne, mawakili wa raia waliiambia Mahakama kwamba jambo muhimu zaidi ni kwamba hakuna kifungu chochote cha Sheria hizo za Serikali za Mitaa kinampa Waziri wa TAMISEMI mamlaka ya kuendesha, kuratibu na kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwamba, Bunge lilipotunga Sheria Namba 2 ya INEC ya mwaka 2024 iliyoipa mamlaka INEC kuhusu mambo yote yanayohusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Bunge hilo lilikuwa linajuwa fika kwamba kuna hizo sheria mbili za Serikali za Mitaa zilizokuwa zinaruhusu TAMISEMI kutunga kanuni, lakini Sheria hiyo Mpya ya INEC itakuwa imeiondolea TAMISEMI mamlaka hayo (Omniscience doctrine).

Tano, mawakili wa raia waliiambia Mahakama kwamba kwa kuwa Waziri wa TAMISEMI ni Mbunge na mwanachama wa chama kimojawapo kinachoshiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, moja kwa moja anakuwa na maslahi na uchaguzi aliotungia kanuni na kuusimamia jambo ambalo ni ubatili.

Hii ni kwa sababu, Waziri alichopaswa kufanya baada ya kutungwa kwa Sheria ya INEC mwaka 2024, badala ya kupoka mamlaka ya INEC alipaswa kuishauri Serikali ipeleke bungeni muswada wa Sheria itakayoratibu uchaguzi ili INEC isimamie uchaguzi huo kama sheria ya INEC inavyotaka.

Lakini Waziri wa TAMISEMI kwa kupoka mamlaka ya INEC kwa kutunga Kanuni za uchaguzi na sasa TAMISEMI inaendelea na zoezi la kuandikisha wapiga kura, ni ushahidi kwamba Waziri wa TAMISEMI ana maslahi kwenye uchaguzi huo.

Mawakili wa raia waliiambia Mahakama kwamba alichofanya Waziri wa TAMISEMI kupoka Mamlaka ya INEC ni kwamba pia kinakiuka Msingi wa Haki ya Asili (Principle of Natural Justice), ambao unasisistiza kwamba mtu mwenye maslahi na kitu fulani hatakiwi kuwa muamuzi kwenye kitu hicho kama kanuni ya Kilatini ya _nemo judex in causa sua inavyosema.

Waziri wa TAMIZEMI ni mwanachama wa CCM na chama chake kinagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kwa hiyo, kama msimamizi mkuu wa uchaguzi huo anaweza kutumia nafasi yake kupendelea chama chake na hivyo mchakato mzima wa uchaguzi huo, kuanzia kutunga kanuni, kuandikisha wapiga kura, upigaji kura, kuhesabu na kutangaza mshindi hakuwezi kufanyika kwa kuzingatia haki kwa wote.

Kwa mfano, tayari kuna malalamiko kuhusu Kanuni za uchaguzi huo, watoto kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura, baadhi vituo kuwekwa kwenye ofisi za chama cha siasa, na raia kutojitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa madai kwamba hawana imani haki itatendeka.

Mawakili wa raia wameiomba Mahakama itumie mamlaka yake iliyopewa kisheria kutoa uamuzi kwa lengo la kuhakikisha chombo pekee chenye mamlaka kisheria kwa sasa (2024) yaani INEC ndicho kitunge Kanuni na kiendeshe, kiratibu na kisimamie uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila kujali gharama ambayo TAMISEMI imeshatumia hadi sasa kwa sababu HAKI haina gharama ni lazima ionekane inatendeka.

Lengo ni kwamba kila raia wa Tanzania mwenye sifa ya kupiga kura apate imani kwamba haki itatendeka na kwa kuamini HAKI itatendeka atajiandikisha na kisha kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka kuongoza kitongoji, kijiji au Mtaa wake.

Sisi raia tunaamini nchi yetu ikipata viongozi bora waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi ulioendeshwa kwa Haki na Uadilifu,kuanzia mwenyekiti wa kitongoji hadi Rais, raia watapata furaha na nchi yetu nzuri Tanzania utainuka.

Mungu Ibariki Tanzania

About The Author