October 30, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

DC Mpogolo aipa tano CBE kwa kuwapa elimu ya bure wajasiriamali

 

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kwa kuanza kuwapa mafunzo ya bure ya ujasiriamali wanawake wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ilala, Dar es Salaam … (endelea).

Ameyasema hayo leo wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 600 wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam yaliyoendeshwa chuoni hapo bure kwa wajasiriamali wanawake.

Mpogolo alisema imekuwa kawaida kwa wajasiriamali wengi wanawake kufanya biashara kwa mazoea bila kuwa na ujuzi wowote lakini mafunzo hayo yamewafungua macho na kupata ujuzi wa namna ya kupata masoko.

Aidha, alisema mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwani wanasiriamali wanawake hao wamepewa elimu kuhusu namna ya kutunza fedha zao, namna ya kutunza mikopo na namna bora ya kurejesha mikopo bila kuwa na msuguano na wale wanaotoa mikopo hiyo.

“Wilaya ya Ilala na Jiji tumefurahishwa na mpango huu wa CBE na Mkurugenzi na timu yake wamefurahishwa sana pia na wanawaunga mkono kwenye mpango huu wa kuwasaidia wajasiriamali,” alisema Mpogopo

Aidha, alisema amezungumza na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga kuangalia namna ya kupeleka elimu hiyo kwenye kata za pembezoni ili wanawake wengi waweze kunufaika na elimu hiyo.

“Nimefurahi sana kuona wamepewa elimu ya mikopo kwasababu kwetu Ilala tumetenga shilingi bilioni 11 kwaajili ya kukopesha wajasiriamali kwa hiyo elimu hiyo waliyopata inatupa uhakika kwamba watafanyabiashara na kurejesha mikopo yao,” alisema

Aidha, Mpogolo alisema kwenye mikopo itakayotolewa serikali imewatenga wajasiriamali hao kwenye makundi matatu kundi la kwanza likiwa lile la wajasiriamali watakaopata mkopo wa kuanzia shilingi 500,000 hadi 10,000,000.

Alitaja kundi lingine kuwa ni lile la wajasiriamali watakaopata mkopo wa kuanzia shilingi 10,000,000 hadi shilingi 50,000,000 wakati kundi la tatu ni la wajasiriamali watakaokopa kuanzia shilingi 50,000,000 hadi shilingi 150,000,000.

“Sisi tumeona tusisitize kundi la kwanza lenye wanawake wengi ambao amekuwa wakichukua mikopo umiza ambao wengi wao wanachukua mikopo ya kuanzia shilingi 20,000, wengine 50,000 na wengine 100,000 au 200,000 wanachukua fedha kidogo sana lakini ni kundi kubwa sana,” alisema

Mkuu wa Chuo cha (CBE), Profesa Edda Lwoga alisema wamekuwa wakitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana na kwaajili ya kuwajengea uwezo ili kuimarisha biashara zao.

“Tunafahamu kwamba kwa kuwajengea uwezo tutakuwa tumewezesha kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa familia na kwa taifa kwa ujumla, leo tumeanza na Ilala kuwajengea uwezo wajasiriamali 600, tumewafundisha namna ya kufungasha biashara, kutafuta masoko, kutunza fedha na kurejesha mikopo kwa wakati,” alisema

Aidha, alisema wamewafundisha pia namna ya kutengeneza mpango bora wa biashara na aliishukuru Wilaya ya Ilala ambayo imeshirikiana kwa karibu na chuo cha CBE kuwapata wajasiriamali hao ambao wamepata mafunzo ya siku tatu.

Alisema mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwenye kampasi za CBE kwenye mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya ambapo wajasirimali 600 wa mikoa hiyo nao watanufaika na mafunzo ya aina hiyo.

Meneja Mafunzo wa benki ya Equity, Martini Rajabu alisema benki hiyoinaona fahari kuungana na CBE kutoa elimu ya ujasiriamali nchi nzima kwani wanawake wengi wanafanyabiashara bila kuwa na ujuzi unaohitajika.

“Sisi tunaamini kuwa wajasiriamali wadogo nchini ndio wanaweza kufanya uchumi wa nchi ukakua kwa kasi kwa hiyo tutaendelea kushirikiana na CBE kuhakikisha idadi kubwa ya wanawake wajasiriamali wanafikiwa na elimu hii,” alisema.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Aneth Bambo ambaye ni mkazi wa Chanika, alimshukuru mkuu wa chuo hicho kwa kuwapa wanawake fursa ya kupata mafunzo hayo ambayo alisema yamewafumbua macho kwenye masuala mbalimbali ya biashara.

“Nawaomba wasiishie hapa kuna wanawake wengi mtaani ambao hawana elimu ya biashara, wawatembelee kwenye biashara zao na kuwapa fursa kama hii kwasababu tunaamini wakipewa mafunzo kama haya wataboresha baishara zao,” alisema

Rachel Mtambo mkazi wa Chanika, alisema wanawake wengi wamekuwa wakisita kuhudhuria mafunzo kama hayo watapotakiwa kwenda lakini yamekuwa na manufaa makubwa kwani hawawezi kubaki kama walivyokuwa kabla ya kupata mafunzo.

“Mara nyingi tunafanya baishara kwa mazoea bila kujua misingi na kanuni bora za uendeshaji wa biashara kwa hiyo hatua hii ya CBE kuona umuhimu wa kutupa mafunzo ni hatua kubwa nay a kupongezwa lakini cha msingi iwe endelevu kwani wanawake ni wengi wanaohitaji elimu hii,” alisema.

Khadija Said kutoka Mbagala, alisema alikuwa akifanyabiashara kienyeji lakini elimu hiyo imempa mwanga wa kuboresha biashara yake na alipongeza CBE na benki ya Equity kwa kutoa elimu hiyo.

“Ila naomba sana elimu hii ingekwenda kata kwa kata hata kwa wauza maandazi na vitumbua kwenye mitaa ili waboreshe biashara zao, mwanamke ni kiwanda kikubwa sana kwa hiyo mwanamke akiwezeshwa uchumi wa familia unaboreka na maisha bora yanapatikana,” alisema.

About The Author