BAADHI ya wapinzani nchini Kenya, wakiongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, wamelaumu Bunge la Seneti kwa kufanya haraka kumuondoa ofisini aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, bila kujitetea. Inaripoti MItandao ya Kimataifa, Nairobi, Kenya … (endelea).
Kalonzo na wenzake wametoa kauli hiyo leo, wakati wakizungumza na waandishi wa habari walipokwenda kumjulia hali Gachagua aliyelazwa katika hospitali ya Karen, baada ya jana kuugua kifua na kulazwa katika hospitali hiyo.
Jana, tarehe 17 Oktoba 2024, Gachagua alitakiwa kuhojiwa na Maseneti, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya kuugua muda mfupi kabla ya kujitetea, huku wakili wake akiomba ‘bosi’ wake apewe muda hadi Jumanne (Oktoba 22) ili ajitetee.
Hata hivyo, Seneti halikuyapa uzito maombi hayo na kuamua kuendelea na hoja ya kumuondoa kiongozi, ambaye Maseneti wamemkutana na makosa matano kati ya 11, yaliyokuwa yakimkabili.
Kutokana na makosa hayo maseneta 43, walipiga kura ya Ndiyo ya kumuondoa ofisini, huku 13 wakipiga kura ya Hapana, hivyo kumuondoa rasmi ofisini na nafasi yake imechukuliwa na Prof. Kithure Kindiki, aliyethibitishwa na Bunge muda mfupi uliopita kwa kupigiwa kura za ndiyo 236.
Katika mkutano wa leo na waandishi wa habari, Kalonzo amesema walitarajia Bunge la Seneti lingeahirisha jambo hilo angalau kwa siku mbili (hadi kesho), ili kumpa fursa Gachagua aliyepo hospitali kwenda kujitetea.
Amesema kwa hali waliyomwona nayo Gachagua, wanaamini angepewa muda hata wa siku mbili angeweza kwenda kujitetea kwa kuwa anaonekana anaendelea vizuri na daktari wake amethibitisha hali hiyo.
“Mimi nilishasema mapema kuwa mambo yatakwenda haraka sana kwenye Bunge na Seneti, hapa tunaona vyombo vyetu vya uamuzi vilivyofunga ndoa na dola, kuna kuminya demokrasia maana mtuhumiwa alitakiwa kupewa fursa ya kujitetea, sikuona sababu ya Bunge la Seneti kutokubali hoja ya kutoa muda zaidi” amesema.
Kalonzo amesema mchakato wa Katiba na wa kidemokrasia umetiwa doa na uamuzi wa Bunge la Seneti ambalo halikumpa fursa, Gachagua kujitetea licha ya kushiriki mjadala huo kuanzia kwenye Bunge hadi jana alipopata ugonjwa.
“Kenya imekosa fursa adhimu ya kuuonyesha ulimwengu tulivyo na Katiba nzuri na wanavyoendesha mambo yao kwa njia ya demokrasia, tungempa fursa halafu tungemuondoa ingekuwa bora,” amesema.
Mwanasiasa Eugine Wamalwa, aliyekuwapo kwenye mkutano huo, amesema Bunge la Seneti limekiuka haki ya kikatiba na kisheria ya kumpa fursa mtu ya kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Ukweli hizi ni siasa chafu za Rais William Ruto na washirika wake, katusaliti na kuminya demokrasia yetu. Hiki alichokifanya kinatuweka kwenye wakati mgumu,” amesema
Wiki iliyopita Bunge la Kenya, lilipiga kura ya kumuondoa madarakani Gachagua baada ya kukubaliana na mashtaka 11, yaliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.
Wabunge 281 waliunga mkono hoja ya kumuondoa kiongozi huyo madarakani huku 44 wakipiga kura kupinga na mmoja akikataa kupiga kura na hivyo kuvuka theluthi mbili ya kura (233), zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa ofisini.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe
Kulikobaki ni CCM tu, wananchi pigeni kura ya hapana