CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo, kimesisitiza kuwa hakijafuta maandamano yake iliyoyaitisha 23 Septemba, kupinga kushamiri kwa vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu,Dar es Salaam … (endelea).
“Maandamano yetu yako palepale. Hatujayafuta na hatutayafuta,” ameeleza Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa chama hicho na kuongeza, “tutaweza kuyafuta, ikiwa tu, matakwa yetu yametimizwa.”
Kauli ya Lissu imekuja siku tatu baada ya jeshi la polisi nchini, kupiga marufuku maandamano hayo yaliyoitishwa na chama cha upinzani, jijini Dar es Salaam.
Msemaji wa Polisi, Kamishena Msaidizi Mwandamizi, David Misime alisema, viongozi wa Chadema waache kuendelea kuwahamasisha wananchi kujihusisha na kile alichokiita, “uhalifu.”
Alisema, Jeshi la polisi limetoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo, kwamba asitubutu kufanya hivyo. Alisema, “maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika.”
Misime amewataka waliopanga kuhudhuria maandamano hayo, kutopoteza muda na gharama zao, kwani yeyote atakayeingia barabarani kuandamana, atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, kauli ya Lissu imekuja huku Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akikitaka chama hicho, kusubiri kufanyika kwa uchunguzi.
Balozi Nchimbi, alilaani vitendo vya utekaji na mauaji nchini na kuongeza kuwa mauaji ya kiongozi wa Chadema, Mohammed Kibao, yanazidi kuwatia hofu wananchi.
Akiongea kwa hisia kali, Nchimbi alisema, “…taifa linapita kwenye mtihani wa hofu miongoni mwa wananchi, na hatuwezi kulipuuza hilo… Mtu yeyote anayehatarisha usalama wa raia, mtu yeyote ama kikundi kinachotekeleza matendo ya utekaji hawawezi kuwa na nia njema na CCM.”
Chadema kupitia mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, alitaja Jumatano iliyopita – tarehe 11 Septemba – kwamba nia ya maandamano hayo, ni kudai uhai wa wanachama na viongozi wake waliopotezwa.
Mbowe alitoa siku kumi – hadi kufikia tarehe 21 Septemba 2024 – akitaka viongozi husika kuwajibika kwa tuhuma za watu kutekwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha na kuonya hilo lisipofanyika wanachama na viongozi wa Chadema wataandamana.
Hatahivyo, Nchimbi anasema msimamo wa Mbowe na Chadema ni ushindi kwa genge la watekaji.
Alisema: “Tumemsikia Mbowe akitoa mud awa mwisho, yaani tarehe 23 serikali isipotaja majina watachukua hatua. Kwa mtu kama Mbowe kama kafikishwa hapo na genge la watekaji, maana yake ni kuwa genge limefanikiwa.”
Alisema: “Matendo ya utekaji yanafanywa na watu wenye nia mbaya ya kufarakanisha taifa. “Jambo la utekaji na mauaji linatoa taswira mbaya kwa CCM. Hivyo hatuwezi kuunga mkono.”
Lakini Lissu anasema, kama chama kilichoko madarakani hakihusiki na vitendo hivyo, kinapaswa kuchukua hatua ya kuilazimisha serikali yake, kuruhusu kuwapo kwa uchunguzi huru kwa nia ya kukomesha vitendo hivyo.
Lissu anasema, Chadema bado kinataka uchunguzi ufanywe na makachero kutoka mashirika ya kijasusi ya kimataifa kama Scotland Yard ya Uingereza, akidai kuwa vyombo vya usalama nchini, ikiwamo jeshi la polisi, ni sehemu ya watuhumiwa.
Wakati mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliyopita, akisisitiza kuwapo kwa maandamo, wafuasi kadhaa wa Chadema, wanaendelea kuhamisishana kupitia mitandao ya kijamii, kufika Dar es Salaam, ili kushiriki maandamano hayo.
“Tukutane Dar es Salaam, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2024,” zinaeleza jumbe mbalimbali zinazotumwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya wanachama, wakiwamo viongozi wakuu wa chama hicho.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe
Gavu aeleza miradi iliyotekelezwa mkoani Geita