March 17, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Meli kubwa nne za mizigo kufungua fursa Ziwa Tanganyika

KUKAMILIKA kwa mradi wa ujenzi wa meli nne kubwa za mizigo katika Bandari ya Karema ni fursa kwa wananchi wa mikoa inayopitiwa na Ziwa Tanganyika ya Rukwa, Katavi, Kigoma na kuongeza kipato cha kaya na Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu…..(endelea)

Ujenzi wa meli hizo ulianza Aprili 2025 na ukitarajiwa kukamilika Julai 2026. Mpaka sasa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 95 huku meli zote zikiwa majini kwa hatua mbalimbali za uhakiki wa mwisho kuanza kutoa huduma.

Oktoba 2023, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilipokea maombi kutoka Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd kutoka China ikiomba kukodishwa eneo katika Bandari ya Karema ili kujenga meli hizo.

Hayo yamesemwa jana na Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema, Anthony Poyo na wakati wa tukio la kuingizwa majini kwa mara ya kwanza meli ya nne ambapo kukamilika michakato wa vibali ukikamilika zitatoa huduma nchi za DR Congo, Zambia, Burundi na Tanzania mnufaika mkuu kutokana na kuwa na bahari.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wawakilishi wa Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd na watumishi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) wakishuhudia meli ikishushwa majini katika Bandari ya Karema, Mkoa wa Katavi.

Poyo amesema kukamilika kwa meli hizo kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani kama Congo, Burundi na Zambia.

Amebainisha manufaa ya meli hizo kwamba unatarajia kuwa na kichocheo cha usafirishaji wa madini kama ya lithium, shaba na dhahabu kutoka eneo la Manono nchini DRC yanayochimbwa na kampuni hiyo ambapo kupitia Manono, Bandari ya Kalemie hadi Bandari ya Kigoma, Dar es Salaam na Tanga zitatumika kabla ya kusafirisha Kwenda nje ya nchi.

Aidha, Poyo amesema kupitia meli hizo, wakulima nao watanufaika kwa mazao ya kilimo pamoja na ajira kwa Watanzania hususan mabaharia ambapo kila meli moja inahitaji si chini ya mabaharia 15.

Pia, Shughuli za usafirishaji, upakiaji wa mizigo, huduma bandarini pamoja na biashara ndogondogo zitakazozunguka bandari hiyo zitapiga hatua.

“Ujenzi wa meli hizi kumetokana na Serikali kufungua fursa ya uwekezaji. Umeleta fursa kwa vijana, mlango wa kiuchumi kwa taifa letu na wananchi mmojammoja,” amesema Poyo.

“Hivi sasa tuna reli ya SGR, wamiliki wa wa malori watanufaika kwa kuchukua mizigo katika bandari hii. Tumehudumia zaidi ya tani 10,000 za mizigo katika bandari hii, hivyo kuja kwa meli hizi kutaongeza zenye uwezo wa kubeba tani 8,000 kwa wakati mmoja unaona jinsi tutakavyopiga hatua kubwa,” amesema Poyo.

Kwa upande wa wakulima na wafanyabiashara, Poyo aamesema utarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda katika masoko makubwa ya kikanda na kimataifa, kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko na kuongeza kipato cha wananchi wa mkoa wa Katavi na maeneo jirani kama ya Kigoma na Rukwa.

Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Anthony Poyo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu meli nne kubwa za mizigo zilizojengwa bandarini hapo na fursa za uchumi ambao nchi itanufaika nao.

Poyo ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan jinsi inavyotekeleza miradi mbalimbali ya bandari na kuimarisha utulivu ambao umesaidia kuchochea maendeleo ya nchi.

Mei 12, 2025, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alifanya ziara Karema kujionea ujenzi wa meli hizo zitainufaisha zaidi Tanzania kwani usafirishaji wa shehena ya mizigo kutoka Bandari ya Kigoma unategemea kutumia miundombinu ya reli zilizopo za MGR na SGR hadi Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

“Sisi ndio tumeunganishwa na bahari, unaweza kuona tupo kwenye eneo la mkakati. Hii kampuni inayojenga hizi meli inachimba madini mbalimbali DRC na hii kwetu ni fursa kwani watayapitisha Kwenda nje ya nchi kupitia kwetu,” amesema Kihenzile.

Alisema kazi kubwa ambayo Serikali inaifanya ni kuhakikisha inaboresha bandari zake, miundombinu ya reli ya kati na ile ya kisasa (SGR) na jengo la abiria kwenye Uwanja wa Ndege Kigoma ili sekta ya usafirishaji iwe bora na isiwe kikwazo kwa wananchi na wawekezaji.

Kihenzile alisema reli ya kati kutoka Tabora – Mpanda hadi Karema ikikamilika itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini hapo hadi Dar es Salaam na malengo ya Serikali SGR itasambaa nchini na hiyo ndiyo dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Meneja Rasilimali Watu kutoka Kampuni ya Ankola Shipyard Co. Ltd ambao ndiyo waliounda meli hizo, Mohammed Mohamed Chande amesema mradi huo ulianza April mwaka jana na ulitarajia kukamilika Julai mwaka huu.

“Mradi umekuja kufungua njia na mlango wa kiuchumi Ziwa Tanganyika. Tunashukuru kwa ushirikiano ambao tuliupata kutoka serikalini na TPA hadi kutuwezesha kumaliza kwa wakati,” amesema.

Amesema fursa za ajira kwa vijana zimepatikana tangu mradi ulipoanza kwani wengi wamepata ujuzi na kuwa na manufaa kwa taifa,” amesema Chande.

Kuhusu changamoto, Chande aamesema wakati wa utekelezaji walikumbana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo waliweza kukabiliana nayo.

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo ya kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo kwani shughuli zao za kilimo, uvuvi na mifugo huenda ikapata masoko ya ndani na nje kwani usafirisaji utakuwepo.

Mkazi wa Karema, Augustino Heneriko amesema wanaishukuru Serikali kwa kuweka mazingira ya uwekezaji hali ambayo inawafanya kuwa na matumaini ya kufungua fursa za kiuchumi kwao weneywe na nchi.

“Tunamshukuru Rais kwa kuifungua nchi, meli hizi ni fursa kwetu kama nchi na uwepo wa bandari hii ni mzuri kwetu sisi tunaozunguka Karema lakini tunaiomba Serikali kuweka msukumo sasa wa ujenzi wa barabara hii ya kutoka Mpanda hadi Karema ikamilike kwani kwa sasa ni mbovu hasa nyakati za mvua,” amesema Heneriko.

Naye Sarafina Kambi ameungana na Heneriko kwenye suala la barabara akisema ikiwa itakamilika itachangiza wasafirishaji na wananchi ambao kwa sasa wanakutana na adha kubwa.

“Tunamwomba Rais aweke msukumo kwenye ujenzi wa barabara, kama ambavyo bandari imekamilika nayo ikamilike ili usafiri na usafirishaji iwe mzuri na sisi wananchi tunufaike zaidi,” amesena Kambi.

About The Author

error: Content is protected !!