March 5, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

UNDP, Uingereza yawakutanisha viongozi wa vyuo vikuu kuchochea Ubunifu na Ujasiriamali Z’bar

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania), kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chuo cha Indian Institute of Technology Madras Zanzibar (IIT Madras Zanzibar), limewakutanisha viongozi wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa mifumo ya ubunifu kutoka Afrika Mashariki kuanzia tarehe 4-6 Machi 2026, katika Mpango wa Kihistoria wa Kubadilishana Wataalamu wa Kitaaluma (Faculty Exchange Programme) unaolenga kuvigeuza Vyuo Vikuu kuwa injini za kuanzisha biashara bunifu changa (startups) na kukuza ujasiriamali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Ingawa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki vinazalisha tafiti nyingi, vipaji na miliki bunifu (intellectual property), ni uvumbuzi mchache unaofanikiwa kuingia sokoni kama biashara endelevu na zenye uwezo wa kukua. Mpango huu unalenga kuziba pengo hili la kimfumo kwa kuimarisha mifumo ya taasisi, vivutio na ushirikiano unaowezesha uanzishaji wa biashara ndani ya taasisi za elimu ya juu.

Ukifanyika chini ya kaulimbiu “Vyuo Vikuu kama Injini za Ubunifu: Kujenga Njia Endelevu kutoka Maarifa mpaka Biashara,” mpango huu unaviweka vyuo vikuu kama nguzo muhimu za ubunifu, uendelezaji wa teknolojia na ukuaji wa biashara. Utekelezaji wake unafanyika kupitia Mradi wa Ubunifu wa FUNGUO, ambao ni mradi wa kimkakati unaofadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Uingereza (FCDO), na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania). Mpango huu unawakutanisha viongozi wa kitaaluma, watengenezaji wa mifumo ya ubunifu na watunga sera ili kuimarisha mifumo inayosukuma mawazo kutoka maabara za utafiti mpaka kuwa biashara zenye uwezo wa kukua.

Jukwaa hilo lilifunguliwa rasmi na Fatma Mabrouk Khamis, Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambaye katika hotuba yake kuu alisisitiza:

“Tunapofungua programu hii, ningependa kusisitiza kuhusu hatua kadhaa za kuchukua. Kwanza, ushirikiano huu uzalishe matokeo halisi ikiwemo tafiti za pamoja, programu za kubadilishana wahadhiri na miradi shirikishi ya ubunifu. Pili, ubadilishanaji wa maarifa uwe sehemu ya kudumu ndani ya mifumo ya vyuo vikuu na sera za kitaifa za ubunifu. Tatu, watunga sera waendelee kuimarisha mifumo ya udhibiti inayounga mkono ujasiriamali na ubunifu. Nne, ubunifu ubaki jumuishi ili kuhakikisha wanawake, vijana na taasisi changa wanapata fursa. Mwisho, mafanikio yapimwe kwa athari halisi — kwa idadi ya biashara bunifu zitakazoanzishwa na ajira zitakazozalishwa,” alisisitiza Khamis.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Godfrey Nyamrunda, Mkuu wa Ofisi Ndogo ya UNDP Zanzibar, Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kimkakati wa mpango huu katika vipaumbele vya maendeleo ya taifa:

“UNDP tunaona vyuo vikuu kama kiunganishi muhimu ndani ya mfumo wa ubunifu wa Tanzania. Kupitia mipango kama FUNGUO, tunawekeza katika mifumo, ushirikiano na nyenzo za kifedha zinazowezesha wabunifu vijana kupiga hatua kutoka wazo mpaka kuwa biashara. Mpango huu wa kubadilishana wahadhiri unaimarisha ajenda hiyo kwa kuviwezesha vyuo vikuu kuwa si wazalishaji wa maarifa tu, bali pia wajenzi wa biashara bunifu zinazoleta ukuaji endelevu na ajira zenye staha,” alisema Nyamrunda.

Akiutambulisha Mpango wa Ushirikiano huo katika Utafiti, Ubunifu na Ujasiriamali, Dk. Jacqueline Owigo, Mshauri wa Utafiti na Ubunifu katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu Afrika Mashariki, Ubalozi Mkuu wa Uingereza jijini Nairobi, alisisitiza umuhimu wa kujenga mifumo imara ya ubunifu kupitia ushirikiano wa kimataifa.

“Kote katika ukanda huu, tumejifunza kuwa mifumo hai ya biashara bunifu haijitokezi kwa bahati mbaya; hujengwa kwa makusudi. Vyuo vikuu vina nafasi ya msingi katika kulea vipaji vya ujasiriamali, kuimarisha njia za kukuza tafiti mpaka kuwa katika uendelezaji wa kibiashara, na kuwaunganisha wabunifu na sekta binafsi pamoja na wawekezaji. Kupitia ushirikiano wa Uingereza–India–Afrika Mashariki, tunajenga jukwaa la kujifunza kwa pamoja na kushirikiana linalowawezesha wabunifu vijana kubadilishana mawazo kuwa suluhisho za ubunifu kwa vitendo,” alisema Dk. Owigo.

Katika hotuba yake ya utangulizi, Profesa Prabhu Rajagopal, Kaimu Mkurugenzi, Chuo cha IIT Madras – Kampasi ya Zanzibar, alisisitiza umuhimu wa Zanzibar kuwa mwenyeji wa tukio hilo:

“Kuandaa programu hii hapa Zanzibar kunaakisi dhamira yetu ya kujenga utamaduni wa ubunifu uliounganishwa kimataifa na unaojibu mahitaji ya ndani. Vyuo vikuu vinapaswa kubadilika kutoka kuwa wazalishaji wa maarifa mpaka kuwa waanzilishi wa biashara hai bunifu. Kwa kutumia motisha, kuimarisha mifumo ya uhamishaji wa teknolojia, na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, tunaweza kujenga njia endelevu kutoka utafiti mpaka biashara; tunatarajia kuona mbeleni wahitimu wanakuwa waajiri, na sio watafuta ajira pekee,” alisema Prof. Rajagopal.

Kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza, ilyiojulikana kama RISE 4.0. Awamu ya Pili ya mpango huu imeyaalika makundi tofauti ya wanafunzi yenye mifano ya bunifu zilizoanza kufanya kazi (prototypes) zinazoshughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi kupitia teknolojia za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (Industry 4.0) kama vile akili bandia (AI), ujifunzaji wa mashine (machine learning), Mtandao wa Vitu (IoT), roboti, blockchain, uchakataji wa kidijitali wa hali ya juu na mifumo ya utabiri.

Programu hii ambayo ilifanyika kwa njia ya mtandaoni ilibuniwa kuyasaidia makundi tofuati ya wanafunzi kuboresha suluhisho zao walizobuni, kuthibitisha mahitaji ya soko na kuonyesha hatua ya utayari wa Bidhaa Inayokubalika Sokoni (Minimum Viable Product – MVP), ikiwa na njia thabiti ya kuelekea kuwa biashara kamili. Suluhisho bunifu zinatarajiwa kutoa ufumbuzi kwenye maeneo ya kipaumbele kama vile nishati safi na jadidifu, kilimo na mifumo ya chakula inayostahimili tabianchi, miji na miundombinu himilivu na mzunguko wa uchumi na urejelezaji taka.

Makundi yatakayofanya vizuri zaidi yatapatiwa mtaji wa awali, fursa ya kujumuishwa katika programu za mafunzo ya ukuaji kupitia taasisi washirika, na kuunganishwa katika mtandao mpana wa ubunifu ili kuimarisha utayari wao wa kupokea uwekezaji na kukuza biashara. Mbali na maboresho ya kiufundi, programu inasisitiza kukidhi soko, msaada wa taasisi na kuunganishwa kimfumo ili kuhakikisha mifano bunifu ya suluhisho bora inageuka kuwa biashara endelevu zenye athari chanya kwa tabianchi.

Sambamba na mafunzo ya siku nne kwa wanafunzi, Mpango wa Kubadilishana Uzoefu utakaofanyika wa siku tatu utawakutanisha viongozi wa kitaaluma kuchambua mifano hai kutoka nchi za kimataifa na kikanda ya uanzishaji wa biashara bunifu, ukijifunza kutoka taasisi kama Indian Institute of Technology Madras na Chuo Kikuu cha Leeds. Majadiliano yataangazia usimamizi wa ubunifu, usimamizi wa miliki bunifu, mifumo ya uhamishaji wa teknolojia, na ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi, yakihitimishwa kwa Maonesho ya Ubunifu wa Wanafunzi na mpango kazi wa utekelezaji wa baadaye.

Kwa pamoja, vipengele vya mada hizi vinakusudia kuimarisha mitandao ya kikanda, kuongeza uwezo wa wahadhiri katika uendelezaji wa teknolojia kibiashara, na kuviweka vyuo vikuu vya Tanzania na Afrika Mashariki kama injini za ukuaji wa ujasiriamali unaochochewa na ajenda ya tabianchi.

About The Author

error: Content is protected !!