February 4, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT – Z’bar yaishukia ZEC sakata la kuchoma nyaraka

 

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar [ZEC] kuacha kuchukua hatua ya kuteketeza nyaraka za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa sababu kufanya hivyo ni kunaashiria kuvuruga mashauri yaliyoko mahkamani yanayohusu kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Vuga mjini hapa leo, Makamu Mwenyekiti Ismail Jussa Ladhu alisema mpango wa Tume ya Uchaguzi unashangaza kwa sababu Tume yenyewe imetumia nyaraka hizo kujibu malalamiko ya waliofungua kesi Mahkama Kuu Zanzibar.

Amesema anatambua kuwepo kwa kifungu 98 katika Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya Zanzibar lakini tume hailazimishwi kuteketeza nyaraka baada ya siku 90 tangu kumalizika kwa uchaguzi.

Jussa amesema hatua ya kuazimia kuteketeza nyaraka za Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni ya aibu na fedheha na pia kituko kwa dhima ya Tume kutoa fursa kwa umma kutimiza matakwa ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

Jana, Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilitangaza rasmi kuwa inatekeleza sheria kwa kuteketeza nyaraka zote za uchaguzi uliopita. Taarifa yao ilisema kifungu cha 98[3] cha Sheria ya Uchaguzi Zanzibar kinaelekeza kuteketeza nyaraka za uchaguzi wakati wowote baada ya kupita siku 90 ulipomalizika uchaguzi.

Shirika la Utangazaji la Zabzibar [ZBC] lilimnukuu Mkuu wa Divisheni ya Sheria, Ame Mohamed, akisema kuwa wanatekeleza matakwa ya sheria hasa kwa kuwa “hakuna zuwio lolote la kisheria.”

Alisema Tume inachukua hatua hiyo baada ya kujadiliana na kushirikisha wadau wa uchaguzi.

Lakini, Jussa amesema sheria hiyo haisemi “ni lazima” kuteketeza nyaraka na akaongeza, “kwa sababu Tume wanajua wenyewe ni walalamikiwa kwenye mashauri ya kupinga matokeo ya uchaguzi waliouandaa na kuusimamia, itateketeza vipi nyaraka wakati kuna kesi zinaendelea mahkamani?”

Amesema mpango huo ambao chama chao hakijashirikishwa, ni dhahiri unakusudia kuharibu ushahidi wa kesi zilizofunguliwa ambako hata wao Tume wamejibu kwenye maombi kuwa fomu za matokeo ni sehemu ya ushahidi wao?

“Ni kosa la jinai kuharibu ushahidi wakati kuna shauri la kisheria linaloendelea… [Tume] inafahamu kwa uhakika nyaraka hizo kwa vyovyote vile zinahitajika mahakamani. Kutumia kifungu cha sheria katika mazingira ambayo Tume inajua imeshitakiwa mahkamani, ni kuonesha nia ovu na kuharibu kwa makusudi ushahidi.

Wanasema wanafuata sheria, lakini tunahoji kama kweli Tume ya Uchaguzi iko makini wa kufuata sheria kama inavyotaka watu waamini, basi leo kusingekuwa na mashauri mahkamani ya kupinga uchaguzi wa majimbo 25 idadi ambayo ni rekodi ya kipekee tokea kufanyika uchaguzi kabla na baada ya mapinduzi 1964,” alisema Jussa.

Alisema: Unapoyachukua mambo haya katika muktadha wake, unagundua dhamira ovu na mchezo mchafu wa kusudio la kukanyaga haki za watu kwa mara pili mara hii ikiwa ni kupitia ucheleweshaji wa haki na uteketezaji wa ushahidi. Baada ya kwanza kuzikanyaga haki hizo kwenye vituo vya kupigia na kuhesabu kura.”

ACT Wazalendo inataka Tume isitishe mpango wake huo mpaka kesi ziamuliwe; Mahkama kupitia kwa Mrajis wa Mahkama Kuu ishughulikie maombi yalioko mezani ya “ukaguzi wa nyaraka (kwani) siku moja ya ukimya wake ni ushirikiano wa kuharibu ushahidi; na kuziomba mamlaka za ulinzi na usalama nchini kuhakikisha nyaraka zote za uchaguzi mkuu 2025 zinatunzwa chini ya ulinzi madhubuti ili kuzuia “moto wa ajali” au upotevu.”

Wagombea waliowakilisha ACT Wazalendo katika majimbo 25, nusu ya majimbo 50 yalioko Unguja na Pemba walifungua kesi Novemba mwaka jana kupinga matokeo. Kesi hizo hazijaanza kusikilizwa.

About The Author

error: Content is protected !!