January 7, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Bagonza achambua wanaopinga Kanisa Katoliki

Askofu Benson Bagonza

 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Benson Bagonza, amelipongeza jeshi la polisi nchini, kuwaruhusu wananchi kutoa maoni yao kwa njia ya maandamano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, kuwaruhusu wananchi kuandamana, ni ukomavu na ustarabu wa hali ya juu uliofanywa na jeshi hilo.

Askofu Bagonza alikuwa akizungumzia hatua ya wanaojiita, “Wakatoliki 100,” waliokwenda ofisi za ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, kulalamikia viongozi wawili wa kanisa hilo, Padre Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Thaddaeus Ruwa’ichi, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Wanaojiita Wakatoliki 100, wanadai kuwa Padre Kitima na Askofu Ruwa’ichi, wanalivuruga kanisa lao kwa kuhubiri chuki na kuliingiza kwenye siasa.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Askofu Bagonza anasema: “Nalazimika kuwapongeza polisi wetu kwa ukomavu wao na ustaarabu wa kutozuia maandamano ya ‘Wakatoliki’ walioenda kueleza hisia zao kwa Balozi wa Papa hapa nchini.

“Nachukulia uvumilivu wao kama ishara ya kuacha kupambana na maoni ya watu na hisia zao. Basi wafute hata kesi za Mzee Mwandambo aliyekamatwa kwa kueleza hisia zake za kidini.”

Dk. Bagonza anasema, “…kumbe, msimamo huu wa Polisi ulianza mapema, pale walipomvumilia kiongozi aliyesema atakata vichwa vya watakaoandamana. Shikilia hapo hapo Polisi, jizuie kuingilia uhuru wa watu na maoni yao.

“Wakatoliki hawa’ wasiojua kusoma vizuri walichokiandaa; walioamua kumwimba “Mwamba ni Yesu” badala ya Bikira Maria Mlinzi wa Taifa letu, na waliosahau kuwa Baba Mtakatifu wa sasa anaitwa Papa Leo wa 14; wametimiza haki yao ya kikatiba.”

Askofu Bagonza ameeleza kuwa “Watakapokuja Wakatoliki halisi wanaojua kusoma na kuvaa kwa heshima mbele ya Balozi wa Papa, wakasoma tamko lao kuwataka Polisi wamkamate aliyempiga Padre Kitima.

“Na wamlete aliyeteka mapadre na kuwadhalilisha, akawavisha wake za watu mavazi ya kitawa ili waonekane ni watawa walioshika bendera za vyama nk – hawa Wakatoliki wakiandamana, polisi kuweni wavumilivu kama mlivyokuwa wavumilivu kwa “Wakatoliki” wale.”

Askofu Bagonza anasema, anaamini kuwa chuki dhidi ya Ukatoliki inayoendeshwa kwa mikakati mibovu, ina nia mbaya dhidi ya serikali kuliko ilivyo na nia mbaya dhidi ya Ukatoliki.

Anaongeza, “Kupigana na Ukatoliki ni lazima uwe na dini nyingine ndani yako inayokusukuma kupigana vita hiyo. Wajaluo “tusiotahiriwa” tunajiuliza hiyo dini ni ipi?”

About The Author

error: Content is protected !!